AFC Leopards itahamisha mechi zake za nyumbani kutoka uwanja wa kitaifa wa Nyayo hadi Ulinzi Sports Complex unaopatikana kando ya barabara kuu ya Lang’ata kwenye Kaunti ya Nairobi.
Mwenyekiti wa klabu hiyo, Dan Shikanda alisema wamelazimika kuchukua hatua hiyo kufuatia mpango wa Serikali kufunga viwanja vya Nyayo na MISC Kasarani ili vifanyiwe ukarabati kulingana na matakwa ya Shirikisho la Kimataifa la Soka
Uwanja wa Ulinzi Sports Complex ulizinduliwa rasmi mnamo Aprili, 2022 na aliyekuwa rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta na umekuwa ukitumiwa kuandaa mashindano mbali mbali ya vikosi vya jeshi, mbali na kutumiwa kuandaa mechi za FKF-PL.
Shikanda alisema Leopards wanakaribia kukamilisha usajaili wa wachezaji kadhaa wapya watakaosajiliwa kabla ya msimu mpya wa 2023/2024 kuanza Agosti 25.
Alisema timu yake inalenga kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Kenya (FKF) baada ya kusubiri tangu 1998.
Kulingana na mwenyekiti huyo, lengo kuu ni kumaliza mabingwa wa ligi msimu ujao, jambo ambalo alisema litawezekana baada ya klabu hiyo kukubaliwa kusajili wapya baada ya marufuku ya FIFA kuondolewa mapema mwezi uliopita.
Leopards hawakuruhusiwa kusajili wachezaji kwa kipindi cha misimu miwili iliyopita baada ya kustakiwa na wachezaji wa zamani wakiwemo Soter Kayumba, Bienvenue Shaka, Alex Kouassi, Gideon Waja na Vincent Habamahoro kutokana na deni.
Baada ya kuwapa matumaini makubwa mashabiki wao, Leopards walichanganyikiwa na hata kushindwa kumaliza msimu miongoni mwa tano bora, huku wakitosheka na nafasi ya saba jedwalini.
Katika mechi za maondoano za Mozzart Cup, Leopards walimaliza katika nafasi ya tatu baada ya kuichapa Ulinzi Stars 1-0 wikendi iliyopita, huku Kakamega Homeboyz wakitwaa ubingwa wa taji hilo baada ya kulaza Tusker 1-0 fainalini
Kwingineko Timu ya Tusker FC inayoshiriki Ligi Kuu ya FKF inatazamia kukamilisha uhamisho wa wachezaji wawili wa Nzoia Sugar James Kibande na Joseph Mwangi, baada ya makubaliano na klabu yao.
Wawili hao wamekuwa wakilengwa kwa muda mrefu na Brewers na walikuwa kwenye hatihati ya kuhamia Ruaraka mwanzoni mwa msimu uliopita – pamoja na kiungo Kevin Juma – lakini walifunga saa kumi na moja kuhusu zamu.
Lakini sasa, yote yanaonekana kuwa tayari kwa wawili hao kujiunga na watengeneza bia.
Kibande alikuwa amerejea Nzoia kwa mkopo baada ya kukosa mafanikio nusu msimu akiwa na timu ya Kenya Police FC.
Watengenezaji bia wanatazamia kukiimarisha kikosi chao kwa kukijenga upya huku wachezaji kadhaa waandamizi wakitarajiwa kuihama klabu hiyo.
Miongoni mwa ambao tayari wameondoka Tusker ni pamoja na beki Mtanzania Kalos Kirenge, mshambuliaji wa Uganda Deogratious Ojok, beki wa kulia Kevin Monyi na kipa Michael Wanjala ambao kandarasi zao tayari zimekatika.
Pia anayetajwa kuondoka klabuni hapo ni kiungo Shami Mwinyi ambaye pia mkataba wake unaelekea ukingoni, huku hatima ya wachezaji wakongwe Jackson Macharia na Humphrey Mieno nayo ikining’inia.
Watengenezaji pombe hao wanatazamiwa kufanyiwa upasuaji mkali baada ya kumalizika vibaya msimu uliopita, ambapo walipoteza taji la ligi siku ya mwisho pamoja na Kombe la FKF kwa Kakamega Homeboyz.