
Taekwondo Character

FLORENCE SIMIYU
Mshindi wa medali ya shaba katika Taekwondo kwenye Michezo ya Afrika, Mary Muriu, amejizatiti kwa malengo ya kufuzu kwa Michezo ya Olimpiki ya Los Angeles 2028.
Muriu, ambaye ni bingwa wa uzani wa manyoya, anajiandaa kushiriki katika mfululizo wa mashindano ambayo yatamfungulia njia ya kufuzu kwa Olimpiki.Katika safari hii, Muriu pamoja na wachezaji wengine watano, wataiwakilisha Kenya kwenye Kombe la Rais wa Taekwondo Afrika litakalofanyika kati ya tarehe 25-27 Aprili mwaka huu katika Addis Ababa, Ethiopia.
Mashindano haya ni sehemu muhimu ya kujenga msingi wa alama za kufuzu kwa Olimpiki.Muriu ameongeza juhudi kubwa katika mazoezi, akilenga kutoa maonyesho bora ili kuhakikisha anapata nafasi ya moja kwa moja kwenye Michezo ya Olimpiki.
Video ya nyota wa Taekwondo,Mary Muriu.[VIDEO COURTESY KBC SPORTS]
Kwa kufikia lengo lake, Muriu anapaswa kuwa miongoni mwa wachezaji watano bora katika uzani wake ifikapo Januari 2028. Baada ya kujizolea pointi 20 kutoka Mashindano ya 7 ya Asia Taekwondo Open alipojizolea dhahabu, anapania kufanya vyema zaidi katika mashindano ya Ethiopia.
Muriu ni sehemu ya Timu ya Kenya, ambayo itakuwa na wachezaji sita wakuu, wakiwemo David Mbogo Nyango, bingwa wa taifa wa uzani wa kati, ambaye anatazamia kuandika historia ya medali katika mashindano yake ya kwanza ya kimataifa.Kocha mkuu Linus Marango ameonyesha imani kubwa katika timu hiyo, akihimiza wadau wa Taekwondo kujitokeza kusaidia timu kugharamia safari yake.Timu inatarajiwa kuondoka tarehe 19 Aprili na mashindano haya yanatarajiwa kuwa na ushiriki wa zaidi ya mataifa 15 kutoka barani Afrika.