Seti za kujipima VVU hukuruhusu kuangalia hali yako nyumbani kwa haraka na kwa faragha kwa sampuli ya damu ya kidole au usufi mdomoni.
BY CYNTHIA ELIZABETH

Serikali imezindua mipango ya kiutendaji ya kudhibiti maambukizi ya
HIV katika kaunti zote 47 kufuatia takwimu mpya kuonyesha kuwa watoto,
balehe na vijana sasa wanachangia zaidi ya nusu ya maambukizi mapya ya
virusi hivyo nchini.
Kwa mujibu wa takwimu za mwaka wa 2026 zilizotolewa na Baraza la
Kitaifa la Kudhibiti Magonjwa ya Syndemic (NSDCC), Kenya ilirekodi
maambukizi mapya 13,936 ya HIV, huku vijana wa balehe wakichangia
asilimia 41 ya maambukizi mapya miongoni mwa watu wazima. Kwa pamoja,
watoto, balehe na vijana wanawakilisha asilimia 55 ya maambukizi mapya
ya HIV nchini.
Takwimu hizo pia zimeonyesha kuwa maambukizi kutoka kwa mama kwenda
kwa mtoto bado yanaendelea kuwa changamoto, yakisalia juu ya kiwango
kinacholengwa kimataifa. Hali hiyo inaashiria kuwa watoto wengi bado
wanapata maambukizi wakati wa ujauzito, kujifungua au kunyonyesha
licha ya uwepo wa huduma za kinga.
Kufuatia hali hiyo, serikali sasa inalenga kupeleka mapambano dhidi ya
HIV karibu zaidi na jamii kupitia mipango ya kiwango cha kaunti badala
ya kutegemea mfumo mmoja wa kitaifa.

Kupitia mikakati hiyo, kila kaunti itatekeleza hatua zinazolingana na
kiwango cha maambukizi katika eneo lake, makundi yaliyo katika hatari
kubwa pamoja na changamoto za upatikanaji wa huduma za kinga, matibabu
na ufuatiliaji wa wagonjwa.
Serikali inaamini kuwa mfumo huo utasaidia kuziba mapengo yaliyopo
katika huduma za afya na kupunguza maambukizi mapya, hasa miongoni mwa
watoto na vijana ambao wanaendelea kuathirika kwa kiwango kikubwa
licha ya hatua zilizopigwa katika miaka ya hivi karibuni.
Kenya imeendelea kutajwa miongoni mwa nchi zilizopiga hatua katika
kupunguza maambukizi ya HIV kwa miaka iliyopita, lakini takwimu hizi
mpya zinaonyesha kuwa juhudi zaidi bado zinahitajika ili kufikia
malengo ya kudhibiti maambukizi mapya kwa makundi yaliyo katika hatari
zaidi.