BY CYNTHIA ELIZABETH

Wanafunzi wa kike katika Kaunti ya Bungoma wamehimizwa kukumbatia na
kukuza talanta zao, hasa katika michezo, kama njia ya kuwawezesha
kujijengea maisha bora na kupanua fursa zao za maendeleo sambamba na
elimu wanayoipata shuleni.
Wito huo umetolewa katika kongamano lililowaleta pamoja wanafunzi
kutoka shule mbalimbali wanaoshiriki mchezo wa mpira wa vikapu, ambapo
viongozi na washirika wa maendeleo walisisitiza umuhimu wa kutumia
michezo kama jukwaa la kujenga ujasiri, uongozi na uwezo wa
kujitegemea kwa wasichana. Kongamano hilo pia lilijumuisha vipindi vya
uhamasishaji na mazungumzo kuhusu maendeleo ya mtoto wa kike.
Akizungumza katika hafla hiyo, Msimamizi wa Wakfu wa Usawa, Elizabeth
Waliuba, alisema kuwa talanta zina nafasi kubwa katika kubadilisha
maisha ya wanafunzi na zinaweza kuwa chanzo cha fursa za baadaye ikiwa
zitapewa mazingira sahihi ya kukuzwa.
Waliuba alibainisha kuwa michezo si tu njia ya kujenga afya na
nidhamu, bali pia inaweza kufungua milango ya ufadhili wa masomo,
maendeleo ya kitaaluma na fursa za ajira kwa wanafunzi wanaoonyesha
uwezo wa kipekee.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mipango Maalum katika Serikali ya
Kaunti ya Bungoma, Caren Wanyonyi, alisema serikali ya kaunti
imeendelea kutoa mwongozo na ushauri nasaha kwa wanafunzi kama sehemu
ya juhudi za kupunguza visa vya mimba za utotoni na kuwahamasisha
kufanya maamuzi yanayowanufaisha katika maisha yao ya baadaye.
Naye Naibu Gavana wa Kaunti ya Bungoma, Jenipher Mbatiany, aliahidi
ushirikiano kati ya serikali ya kaunti na washirika mbalimbali ili
kuendelea kuboresha elimu pamoja na mazingira yanayomwezesha mtoto wa
kike kustawi katika nyanja za masomo, michezo na maendeleo ya kijamii.
Washiriki wa kongamano hilo pia walihimizwa kuendelea kujiamini,
kutumia vipaji vyao ipasavyo na kutambua kuwa elimu na talanta
vinaweza kwenda sambamba katika kujenga mustakabali bora.