![Picha ya Waziri wa Michezo na Masuala ya Vijana Salim Mvurya [PICHA, ALEX WEKESA TANDAO MEDIA GROUP]](https://tandaomedia.co.ke/wp-content/uploads/2025/03/LUSAKA-2.jpg)
Picha ya Waziri wa Michezo na Masuala ya Vijana Salim Mvurya [PICHA, ALEX WEKESA TANDAO MEDIA GROUP]
![Picha ya Waziri wa Michezo na Masuala ya Vijana Salim Mvurya [PICHA, ALEX WEKESA TANDAO MEDIA GROUP]](https://tandaomedia.co.ke/wp-content/uploads/2025/03/LUSAKA-2.jpg)
BY ALEX WEKESA, TMG JOURNALIST.
Serikali ya kitaifa kupitia Wizara ya Michezo na Masuala ya Vijana imezindua mfumo mpya wa kuwasikiza vijana maarufu kama Wazo Engagement Forum.Uzinduzi huo ulifanyika katika Chuo Kikuu cha Kibabii, kilichopo katika kaunti ya Bungoma, ambapo Waziri Salim Mvurya alieleza kuwa mfumo huo utawasaidia vijana nchini kote katika kushiriki katika maamuzi yanayowahusu.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Waziri Mvurya alisema kuwa mfumo wa Wazo Engagement Forum utaendelezwa katika kaunti zote 47, ikiwapa vijana fursa ya kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na washikadau kutoka sekta tofauti za serikali.
Alisisitiza kuwa lengo la jopo maalum lililoanzishwa ni kuhakikisha kuwa masuala ya vijana yanashughulikiwa kwa umakini, na kwamba kushirikiana na maafisa wa nyanjani kutasaidia katika kufikia malengo hayo.Waziri Mvurya pia alikiri kwamba vijana wengi nchini hawana ufahamu wa fursa zilizopo za kiuchumi, akiongeza kuwa mfumo huu utaimarisha uelewa wao na kuwapa motisha ya kuchangamkia nafasi hizo.Alisisitiza umuhimu wa vijana kujiunga na mfumo huo ili waweze kutimiza ndoto zao za kimaisha.
Kwa upande wake, Gavana wa Bungoma, Kenneth Lusaka, aliwahimiza vijana wajiunge katika makundi ili waweze kufaidika na mipango mbalimbali ya serikali.Lusaka alionyesha umuhimu wa kuwapa vijana elimu kuhusu mikopo ya serikali inayolenga kuwasaidia katika kuanzisha biashara na shughuli zao.

Aliwataka vijana kutumia mikopo hiyo kwa njia inayofaa ili kuweza kujenga mustakabali bora.
Gavana Lusaka alikiri kwamba wengi wa vijana wana changamoto ya mtaji wa kuanzisha biashara na aliahidi kwamba serikali itashirikiana na benki ili kuwawezesha vijana kupata msaada wa kifedha.
Uzinduzi wa Wazo Engagement Forum unatarajiwa kuleta mabadiliko chanya katika ushirikishwaji wa vijana katika masuala ya maendeleo na ujasiriamali nchini.Serikali inaweka mipango ya kuimarisha uhusiano kati ya vijana na serikali ili kuhakikisha kuwa sauti zao zinakubalikaย naย kutekelezwa.