
Picha ya Wycliffe Oparanya,waziri wa Vyama vya Ushirika na Maendeleo ya Biashara Ndogo, Ndogo na zaย Katiย (MSMEs).

TANDAO MEDIA – Katika kile walichokiita “Azimio la Khwisero,” Wabunge wa eneo la Magharibi wameonyesha uungaji mkono wao kwa Waziri wa ushirika,Wycliffe Oparanya wakisema kuwa ana sifa za kipekee za kuwa Naibu wa Rais.Viongozi hao wakiongozwa na Mbunge wa Khwisero- Christopher Aseka na Mbunge wa Lurambi Askofu Titus Khamala, wamesema kuwa wakati umefika kwa eneo hilo kujitokeza na kushiriki kikamilifu katika nafasi za juu za uongozi.
Viongozi hao wanasema kuwa rekodi ya Oparanya, ikiwemo kipindi chake kama Gavana wa kwanza wa Kaunti ya Kakamega na nafasi yake kama Mwenyekiti wa Baraza la Magavana, inamfanya kuwa kiongozi wa kipekee katika siasa za kitaifa. Wakisisitiza kuwa idadi kubwa ya jamii ya Waluhya inastahili nafasi katika maamuzi ya kitaifa.

Oparanya, ambaye kwa sasa anahudu kama Waziri wa Ushirika na maendeleo ya biashara ndogo ndogo zaidi na za kati, alianza safari yake ya kisiasa mwaka wa 2002 alipoteuliwa kuwa Mbunge wa Eneo Bunge la Butere. Baadaye mwaka wa 2008 alihudumu kama Waziri wa mipango na Dira ya Maendeleo ya 2030 chini ya Rais wa zamani hayati Mwai Kibaki, kabla ya kuchaguliwa kuwa Gavana wa Kakamega kutoka mwaka wa 2013 hadi mwaka wa 2022.
Msimamo huu wa pamoja unaashiria juhudi za kimkakati za kuinua ushawishi wa eneo la Magharibi katika jukwaa la kitaifa, huku viongozi wakihakikisha sauti zao zinasikika katika kuunda mustakabali wa Kenya.