Picha inayoonyesha mwanamke mlemavu kwenye wati la gurudumu akizungukwa na watu njiani. PICHA: KWA HISANI

BY DINA ROSE
Watu wanaoishi na ulemavu kutoka Eneo Bunge la Malava, Kaunti ya Kakamega, wameeleza masikitiko yao wakidai kupuuzwa na viongozi baada ya uchaguzi. Wamesema licha ya kushirikishwa kikamilifu wakati wa kampeni, mara nyingi husahaulika na hawajumuishwi ipasavyo katika mipango ya maendeleo.
Wakizungumza mjini Webuye baada ya kuandaliwa chakula cha mchana na mwanahabari John Wanyama, walemavu hao walisema wanasiasa huwatafuta wakati wa kampeni lakini hushindwa kutimiza ahadi walizotoa baada ya kushinda. Mwenyekiti wa kundi hilo, John Shayo, alisisitiza haja ya kuanzishwa miradi mahsusi itakayowawezesha na kuwajumuisha katika maendeleo ya jamii.
Baadhi ya wanajamii walimpongeza Wanyama kwa mchango wake wa kuwasaidia makundi yaliyo hatarini na kuwataka viongozi wengine kuiga mfano huo. Walisema msaada wa kudumu na utambuzi rasmi ni muhimu ili kukabiliana na changamoto za kijamii na kiuchumi zinazowakabili.
Kwa upande wake, Wanyama alieleza kuwa aliamua kuchukua hatua kwa sababu walemavu wamesahaulika kwa muda mrefu. Alisisitiza umuhimu wa kuwasaidia kupata bima ya afya na vyeti rasmi vya utambuzi wa ulemavu ili waweze kunufaika na programu za serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali.