Wataalamu Wahimiza Kilimo cha Mboga za Kiasili.AI-Generated Image. TMG Stock
BY MAGDALINE LUBISIA

Wataalamu wa lishe na kilimo nchini Kenya wametoa mwito kwa wananchi kukumbatia ukulima na ulaji wa mboga za kiasili, wakisema hatua hiyo ni suluhisho la haraka kwa kupambana na umaskini na utapia mlo unaoathiri jamii nyingi.
Ushauri huo ulitolewa katika Kaunti ya Trans Nzoia wakati wa uzinduzi wa mradi wa mboga za kiasili katika Shule ya Upili ya Kitale School. Mradi huo unalenga kuboresha maisha ya wanafunzi kupitia lishe bora na kilimo endelevu kinachoweza kuigwa kote nchini.
Wataalamu walieleza kuwa mboga za kiasili zina viwango vya juu vya virutubisho vinavyosaidia kuimarisha kinga ya mwili na kupunguza magonjwa yanayochangiwa na ulaji wa vyakula visivyo na lishe kamili. Aidha, walisisitiza kuwa kilimo cha mboga hizi ni fursa ya kiuchumi kwa wananchi kutokana na muda mfupi wa kukomaa na mahitaji makubwa sokoni.

Mradi huo unatarajiwa kuwa mfano wa kuigwa, ukihakikisha wanafunzi wanapata milo yenye afya shuleni na kujifunza kwa vitendo mbinu za kilimo cha mboga za kiasili. Walimu na wanafunzi walieleza matumaini yao kuwa mradi huo utaboresha afya na kuongeza uelewa kuhusu lishe bora.
Wataalamu wametoa wito kwa serikali kuu, serikali za kaunti na wadau wa sekta ya kilimo kuendeleza mikakati ya kuhamasisha wananchi kupanda na kula mboga za kiasili, wakisema hatua hiyo itainua afya na viwango vya maisha ya jamii kwa ujumla.