Gavel katika chumba cha mahakama. PICHA/FILE
BY SYPHROSE NAFULA

Mahakama ya Kisii, kwa ushirikiano na Jeshi la Polisi, imesimamia zoezi la kuteketeza bidhaa za mihadarati zilizokuwa zimehifadhiwa chini ya ulinzi mkali tangu mwaka 2018. Zoezi hilo lilifanyika baada ya kukamilika kwa taratibu zote za kisheria, likiwa sehemu ya juhudi za kuhakikisha vielelezo vya kesi vinaharibiwa kwa mujibu wa sheria na haviwezi kurejeshwa katika mzunguko wa matumizi.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Hakimu Mkuu wa Mahakama ya Kisii, Mildred Obura, alisema uteketezaji huo unaashiria mwisho rasmi wa mchakato wa uhifadhi wa vielelezo hivyo mahakamani. Alieleza kuwa hatua hiyo inaonyesha utekelezaji wa sheria kwa uwazi na uwajibikaji baada ya kesi husika kukamilika.
Obura alibainisha kuwa uteketezaji wa bidhaa hizo unasaidia kujenga imani ya wananchi katika mfumo wa haki kwa kuthibitisha kuwa mihadarati inayonaswa na vyombo vya usalama hushughulikiwa kwa mujibu wa sheria hadi kuharibiwa kabisa. Alisisitiza kuwa utaratibu huo unazuia uwezekano wa bidhaa hatari kurejeshwa mitaani na kuhatarisha maisha ya wananchi.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Kisii, Ronald Kirui, alipongeza ushirikiano uliopo kati ya idara ya mahakama na vyombo vya usalama katika mapambano dhidi ya biashara haramu ya dawa za kulevya. Alisema ushirikiano huo umeimarisha juhudi za kuhakikisha walanguzi wanakamatwa, kufikishwa mahakamani na vielelezo vinashughulikiwa kwa kufuata sheria.
Kirui pia aliwataka wananchi kushirikiana kwa karibu na maafisa wa usalama kwa kutoa taarifa kuhusu watu wanaojihusisha na biashara ya mihadarati. Alisema ushirikiano wa umma ni silaha muhimu katika kudhibiti usambazaji wa dawa za kulevya na kuwafikisha wahusika mbele ya sheria.
Aidha, Kamanda huyo alionya kuwa dawa za kulevya zinaendelea kuwa tishio kubwa kwa jamii, hasa kwa vijana, kwa kuathiri afya yao ya akili na kupunguza nguvu kazi ya taifa. Alisisitiza kuwa vita dhidi ya mihadarati vinahitaji ushirikiano wa kila mdau ili kulinda kizazi cha sasa na cha baadaye dhidi ya athari za matumizi na biashara ya dawa hizo haramu.