BY CYNTHIA ELIZABETH

Wagonjwa wanaoishi na virusi vya HIV katika kaunti ya Kakamega wametoa
wito kwa serikali ya kaunti kurejesha maeneo maalum ya kupokea dawa
kama ilivyokuwa hapo awali, wakisema mfumo wa sasa wa kuwahudumia
pamoja na wagonjwa wengine umechangia ongezeko la unyanyapaa.
Wito huo ulitolewa wakati wa kikao kilichowaleta pamoja wanajamii
wanaoishi na virusi vya HIV kwa lengo la kujadili mbinu za kuboresha
utoaji wa huduma na kuhakikisha wagonjwa wanapata matibabu kwa usalama
na kwa kuzingatia faragha yao.
Kwa mujibu wa baadhi ya washiriki, utaratibu wa awali uliwawezesha
kupata huduma katika mazingira yaliyowapa nafasi ya kuzungumza kwa
uhuru na wahudumu wa afya, watoa ushauri nasaha pamoja na waelimishaji
rika kuhusu changamoto wanazokumbana nazo.
Hata hivyo, wanasema mfumo wa sasa wa kuwajumuisha na wagonjwa wengine
katika hospitali mbalimbali umesababisha baadhi yao kusita kwenda
kuchukua dawa kutokana na hofu ya kutambuliwa na kunyanyapaliwa.
Mbali na suala la unyanyapaa, wagonjwa hao pia walieleza changamoto ya
upungufu wa dawa katika baadhi ya vituo vya afya pamoja na uhaba wa
wahudumu wa afya, hali ambayo kwa mujibu wao inaathiri upatikanaji wa
huduma kwa wakati.
Kwa upande wao, maafisa wa afya walisema serikali ya kaunti inaendelea
kuhakikisha dawa muhimu zinapatikana katika vituo vya afya na
kusisitiza kuwa huduma zinazotolewa zinazingatia usawa kwa wagonjwa
wote.
Wagonjwa hao sasa wanaitaka serikali kuimarisha mifumo ya utoaji
huduma ili kulinda faragha yao na kupunguza visa vya unyanyapaa
vinavyoweza kuathiri mwendelezo wa matibabu.