BY CYNTHIA ELIZABETH

Seneta wa Kaunti ya Bungoma David Wakoli ameikosoa serikali ya kaunti
hiyo kwa kile alichokitaja kuwa mapungufu makubwa katika utoaji wa
huduma za afya katika vituo mbalimbali vya matibabu vya eneobunge la
Tongaren.
Akizungumza baada ya ziara ya ukaguzi katika Vituo vya Afya vya Ndalu,
Makutano na Tongaren Model, seneta huyo alisema kuwa vituo hivyo
vinakabiliwa na changamoto zinazohusisha upungufu wa wahudumu wa afya,
ukosefu wa dawa, huduma duni za dharura pamoja na ukosefu wa vifaa
muhimu vya uchunguzi wa magonjwa.
Kwa mujibu wa Wakoli, ziara hiyo ilibaini hali ya kudorora kwa
miundombinu ya afya na mapungufu ya kiutendaji ambayo, kwa maoni yake,
yanaendelea kuathiri upatikanaji wa huduma bora za matibabu kwa wakazi
wa eneo hilo.
Katika Kituo cha Afya cha Ndalu, seneta huyo alidai kuwa ujenzi wa
wodi ya wajawazito ulioanzishwa mwaka wa elfu mbili ishirini na nne
umekwama baada ya mkandarasi kuondoka katika eneo la mradi kabla ya
kuukamilisha. Alisema hali hiyo imeathiri juhudi za kuboresha huduma
za afya ya uzazi kwa wakazi wa eneo hilo.
Aidha, katika Kituo cha Afya cha Makutano kilichopo wadi ya
Soysambu/Mitua, Wakoli alidai kuwa miradi ya ujenzi wa idara ya
wagonjwa wa nje pamoja na wodi ya wajawazito imekwama kwa muda mrefu.
Pia alieleza wasiwasi kuhusu ukosefu wa ambulensi, changamoto za
usalama wa kituo pamoja na usimamizi wa vifaa vya matibabu.
Katika Kituo cha Afya cha Tongaren Model, seneta huyo alieleza kuwa
ukaguzi huo ulibaini changamoto zaidi ikiwemo ukosefu wa baadhi ya
vifaa vya maabara, udhaifu katika usimamizi wa kumbukumbu pamoja na
changamoto zinazohusiana na uhifadhi na utupaji wa taka za matibabu.
Kutokana na hali hiyo, Wakoli amemtaka Afisa Mkuu wa Kaunti
anayehusika na afya kutembelea vituo hivyo binafsi, kuimarisha
usimamizi wa huduma na kuharakisha utekelezaji wa miradi iliyokusudiwa
kuboresha huduma za afya kwa wananchi wa Tongaren.