BY LUCY MUSENYA

Mamlaka ya Kitaifa ya Kusimamia Ukame imetangaza kuwa kaunti zote nchini Kenya zimeingia katika awamu ya kawaida ya ukame, hatua inayoleta afueni kwa jamii za wafugaji zilizokuwa zikabiliwa na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Tangazo hilo ni tofauti na hali iliyoshuhudiwa mapema mwaka huu ambapo kaunti kama Mandera, Wajir, Kwale na Kilifi zilikuwa katika awamu ya Hatari Kuu. Hali hiyo ilikuwa imewaweka zaidi ya Wakenya milioni 3.3 katika hatari ya njaa na utapiamlo kabla ya mvua za masika kuzuia janga hilo. Licha ya hali ya sasa, Afisa Mkuu Mtendaji wa NDMA, Huka Wario, amewataka wadau kubaki macho kwa kuwa baadhi ya maeneo bado yanaweza kurudi katika awamu ya tahadhari ndani ya miezi miwili iwapo hatua hazitachukuliwa.
Serikali imesema inakimbiza utekelezaji wa miradi ya muda mrefu ya maji ili kujikinga na ukali wa hali ya hewa. Katika hatua moja ya hivi karibuni, NDMA ilishirikiana na serikali ya Kaunti ya Garissa kukarabati Kisima cha Arera kwa gharama ya shilingi milioni 1.7. Kisima hicho sasa kinaendeshwa kwa nishati ya jua badala ya jenereta za dizeli, na kimejumuisha matanki ya kisasa na mabwawa ya kunyweshea mifugo.

Mfumo mpya una uwezo wa kuhudumia boma 200 na mifugo zaidi ya 4,000 kwa gharama ya chini, huku ukihakikisha huduma inaendelea hata kipindi cha kiangazi. Wakazi wamesema mradi huo umerahisisha maisha yao na kulinda elimu ya watoto ambao sasa wanabaki shuleni badala ya kutembea umbali mrefu kutafuta maji. By Lucy Musenya