

Alizaliwa mnamo Disemba tarehe 22 katika eneo la Kiminini kaunti ya Trans Nzoia.Ni mmoja wa jamii pana ya Luhya na muda wake mwingi aliishi kaunti ya Bungoma.Alianza masomo yake ya shule ya upili katika shule ya wavulana ya st Peter’s Mumias na ile ya upili ya Bokoli,Kisha akatamatisha masomo hayo,kwa shule ya upili ya Lenana jijini Nairobi.
Baadaye alijiunga na chuo kikuu Cha Nairobi alikosomea Uanasheria na kufuzu mwaka wa 1985.Kabla ya kuwa Mwenyekiti wa Tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC , Chebukati alikuwa mwanasiasa ambapo mwaka wa 2007 aliwania kiti Cha ubunge eneo la Saboti kaunti ya Trans Nzoia kwa tiketi ya chama Cha ODM kilichoongozwa na aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga ila akapoteza kiti hicho baada ya Eugine Wamalwa wa PNU kushinda uchaguzi huo.

Chebukati alijiondoa katika maswala ya siasa na hata kujiuzulu kama mwanachama wa ODM.Januari mwaka wa 2017 aliteuliwa kama Mwenyekiti wa IEBC na aliyekuwa Rais wakati huo Uhuru Kenyatta.Alichukua nafasi ya mtangulizi wake Ahmed Isack Hassan.Uongozi wake kwa miaka sita kama mwenyekiti wa IEBC, ulikumbwa na changamoto tele ambapo katika chaguzi za 2017, Wafula Chebukati alimtangaza Rais Uhuru Kenyatta kama mshindi wa uchaguzi huo ambapo mahakama iliamuru uchaguzi huo kurudiwa kwa kuwa ulikumbwa na udanganyifu.
Baadae Rais Uhuru Kenyatta aliibuka mshindi baada ya kiongozi wa ODM Raila Odinga kususia uchaguzi.Msukosuko wa uchaguzi huo ulipelekea kuwepo mpasuko ndani ya uongozi wa IEBC, ambapo kamishna Roselyn Akombe alijiuzulu na pia kuondoka kwa afisa mkuu Ezra Chiloba.Chaguzi za 2022 mwezi Agosti, Chebukati alimtangaza Rais William Ruto kama mshindi wa urais kwa kupata asilimia 50.49 dhidi ya Odinga aliyepata asilimia 48.85 ya kura zilizopigwa.Chaguzi hizo pia zilipelekea mpasuko ambapo kulionekana makamishna wanne (Cherera four) kujitenga na matokeo ya Urais ila mahakama ikasitiri ushindi wa Rais William Ruto. Wandani wa Rais William Ruto walionekana kumsifia Chebukati kama Mwanademokrasia shupavu kutokana na msukosuko uliokuwa unakumba upeperushaji wa matokeo ya uchaguzi huo.