![Picha ya uwanja wa kimataifa wa Kirigiti kwenye Kaunti ya Kiambu [PICHA FACEBOOK]](https://tandaomedia.co.ke/wp-content/uploads/2025/03/KIRIGITI.jpg)
Picha ya uwanja wa kimataifa wa Kirigiti kwenye Kaunti ya Kiambu [PICHA FACEBOOK]
![Picha ya uwanja wa kimataifa wa Kirigiti kwenye Kaunti ya Kiambu [PICHA FACEBOOK]](https://tandaomedia.co.ke/wp-content/uploads/2025/03/KIRIGITI.jpg)
BY EMMANUEL WABOMBA, TMG JOURNALIST.
Katika hatua muhimu kwa maendeleo ya michezo nchini Kenya, Waziri wa Michezo, Salim Mvurya, ametangaza kuwa ujenzi wa Uwanja wa Kirigiti, ulioko Kaunti ya Kiambu, unakaribia kukamilika. Mvurya amesema ujenzi huo wa kiwango cha kimataifa utakamilika ndani ya siku 45 zijazo.Uwanja wa Kirigiti unatarajiwa kuwa kitovu cha mazoezi kwa Mashindano ya CHAN yanayotarajiwa kufanyika Agosti mwaka huu. Zaidi ya hayo, umechaguliwa kuwa moja ya viwanja vitakavyotumika kwa Mashindano ya AFCON, hatua inayoinua hadhi ya Kenya kwenye tasnia ya michezo ya bara Afrika.
Katika nyanja nyingine za michezo, Kenya imetangaza kwa fahari kikosi cha wanariadha kumi bora watakaoshiriki Mashindano ya Dunia ya Ndani, yatakayofanyika Nanjing, China, kuanzia Machi 21 hadi Machi 23.Kwa upande wa wanawake, timu hiyo inaongozwa na bingwa wa kitaifa wa mbio za mita 800, Lilian Odira ambaye atashirikiana na Vivian Chebet, Purity Gitonga, Dorcas Ewoi, na mwanariadha wa Olimpiki, Susan Ejore.

Kikosi cha wanaume pia kina nyota kama Noah Kibet, ambaye ataongoza mbio za mita 800, akisaidiana na Collins Kipruto na Alex Ngeno.Wanariadha wengine ni Festus Langat, anayewania ushindi kwenye mbio za mita 1,500, na Cornelius Kemboi, anayejitahidi kushinda taji kwenye mbio za mita 3,000.Timu hii inajivunia uwezo wa kuleta ushindi mkubwa huku ikitetea sifa ya Kenya katika ulingo wa kimataifa.
Wakati huo huo, zaidi ya wanariadha 200 wa gofu wanatarajiwa kushiriki awamu ya nne ya Msururu wa Gofu wa NCBA, utakaofanyika kesho katika uga wa gofu Kiambu.Ushindani unatarajiwa kuwa mkali, hasa kwenye shimo la 8, ambapo mpigo maarufu wa โhole-in-oneโ unaweza kumpa mshindi zawadi kabambe ya Backhoe Loader.NCBA, waandaaji wa msururu huo, wanasema mashindano haya yamekuwa muhimu kwa kukuza mchezo wa golfu nchini Kenya.