

Baada ya kifo chake(Papa Francis), Kanisa Katoliki litaanza mchakato wa uchaguzi wa Papa mpya kupitia mkutano wa siri wa makardinali, unaojulikana kama “conclave”. Mkutano huu utafanyika katika Kanisa la Sistine ndani ya Vatican, ambapo makardinali walio chini ya umri wa miaka 80 watajifungia hadi watakapomchagua Papa mpya kwa kura ya siri.
Kwa sasa, kuna makardinali 135 walio na haki ya kupiga kura, wengi wao wakiwa walioteuliwa na Papa Francis mwenyewe.Mchakato wa uchaguzi unahitaji mshindi apate theluthi mbili ya kura zote. Baada ya uchaguzi, moshi mweupe utatoka kwenye bomba la moshi la Kanisa la Sistine, kuashiria kwamba Papa mpya amechaguliwa, na tangazo la “Habemus Papam” litatolewa kwa umma.Kifo cha Papa Francis ni tukio la kihistoria kwa Kanisa Katoliki na dunia inasubiri kwa hamu kuona ni nani atakayemrithi katika nafasi hii ya juu ya kiroho.

Wakatoliki wanaamini kwamba Papa ndiye mwakilishi wa moja kwa moja wa Yesu Kristo duniani;Na anachukuliwa kuwa mrithi hai wa Mtakatifu Petro, kiongozi wa kwanza wa mitume wa Kristo. Ingawa waumini wengi hutafuta mwongozo kutoka kwa Biblia, mafundisho ya Papa pia huchukuliwa kuwa dira ya imani na mila za Kanisa Katoliki.
Papa Francis, ambaye aliongoza Kanisa Katoliki kwa miaka 12 tangu kuchaguliwa kwake mwaka 2013, alifariki dunia mnamo Aprili 21, 2025, akiwa na umri wa miaka 88. Kifo chake kilitokea katika makazi yake ya Domus Sanctae Marthae, Vatican, baada ya kuugua kwa muda mrefu kutokana na matatizo ya kupumua na matatizo ya moyo.
Katika maisha yake, Papa Francis alijulikana kwa unyenyekevu na maisha ya kawaida. Alikataa anasa za kipapa na kuishi maisha ya kawaida, akichagua kuzikwa katika kanisa la Santa Maria Maggiore badala ya Vatican. Mazishi yake yalipangwa kuwa ya kawaida, akitaka jeneza la mbao lililowekwa zinki na kutoonyeshwa hadharani kwa mwili wake.