

By Felix Wanjala .
Serikali ya Rais William Ruto inazidi kukabiliwa na mawimbi ya kisiasa kutoka kwa vijana,viongozi wa upinzani na migawanyiko ndani ya serikali ya ushirikiano(broad-based government).
Baadhi ya wandani wa Rais Ruto wakiongozwa na msaidizi wake wa karibu Farouk Kibet, wamemshutumu rais mstaafu Uhuru Kenyatta wakidai kwamba anahusika katika kuchochea vijana kupinga utawala wa sasa.
Wakati hayo yakijiri, mvutano umeibuka ndani ya chama cha ODM miezi michache baada ya kuingia kwenye ushirikiano na serikali. Mwenyekiti wa chama hicho ngazi ya kitaifa, Gavana Gladys Wanga ametishia kwamba ODM huenda ikaondoka kwenye ushirikiano huo iwapo serikali haitatoa taarifa ya kina na ya kuaminika kuhusu mauaji ya Mbunge wa Kasipul, Charles Were.
Hata hivyo baadhi ya viongozi wa ODM, wandani wa karibu wa Raila Odinga, wanaendelea kusisitiza kuwa chama hicho kinaunga mkono ushirikiano na serikali huku wakitoa hakikisho kwamba Rais Ruto atapata muhula wa pili mwaka wa 2027.
Kauli tofauti kutoka kwa viongozi hawa zimezua mkanganyiko miongoni mwa wafuasi wa chama cha ODM kuhusu msimamo rasmi wa chama. Hali inasalia kuwa ya kusubiriwa ili kufahamu ikiwa ODM itamuunga mkono Rais Ruto kuwania tena urais, kumchagua mgombea mwingine wa upinzani au kama Raila Odinga mwenyewe atajitosa katika kinyangโanyiro hicho mwaka 2027.