

By Felix Wanjala.
Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetangโula leo mapema aliongoza viongozi mbalimbali wakiwemo wabunge kuutazama mwili wa aliyekuwa Mbunge wa Kasipul, Charles Ongโondo Were, katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Lee jijini Nairobi.
Spika Wetangโula ameyataka mashirika yote ya usalama kuanzisha uchunguzi wa kina na wa haraka ili kuwakamata na kuwachukulia hatua kali za kisheria wale wote waliohusika na mauaji hayo ya kinyama.
Baadaye viongozi hao walielekea nyumbani kwa marehemu katika eneo la Karen kuungana na familia katika maombolezo. Mjane wa marehemu, Bi. Margaret Were, ameeleza masikitiko yake akibainisha kuwa marehemu ameacha familia changa na ametoa wito kwa uongozi wa Bunge kusaidia familia hiyo katika kipindi hiki kigumu.

Kwa upande wake, Seneta wa Kaunti ya Nairobi na Katibu Mkuu wa chama cha ODM, Edwin Sifuna, ameitaka serikali kuhakikisha haki inatendeka kwa familia ya marehemu.Sifuna ametaja mauaji ya Mbunge Were kuwa kitisho kikubwa kwa usalama wa viongozi nchini.
Tukio hilo la kusikitisha lilitokea jioni ya Aprili tarehe 30, 2025 majira ya saa 1:30 usiku katika Barabara ya Ngong, jijini Nairobi. Marehemu alipigwa risasi akiwa ndani ya gari lake na mshukiwa aliyekuwa abiria kwenye pikipiki alitekeleza shambulio hilo kabla ya kutoweka. Licha ya juhudi za kumfikisha hospitalini haraka, Mbunge Were alithibitishwa kufariki dunia alipowasili hospitalini.