

By Emmanuel Barasa.
Katika Kaunti ya Kajiado, wanaharakati wa haki za binadamu wameandaa mkutano maalum baina yao na maafisa wa polisi pamoja na watumishi wa serikali, wakilenga kuimarisha ushirikiano na kushirikisha jamii katika masuala ya maendeleo bila kuogopa unyanyasaji au vitisho.
Mkutano huo uliofanyika leo, uliwaleta pamoja wanaharakati kutoka mashirika mbalimbali ya kijamii, ambao walieleza wazi masikitiko yao kuhusu jinsi wanavyonyanyaswa na kutishiwa wanapotekeleza majukumu yao ya kutetea haki za wananchi.
Wanaharakati hao wametaka kuwepo kwa uwazi na mawasiliano ya moja kwa moja kati yao na serikali, wakisema kuwa ukosefu wa maelewano umekuwa ukisababisha migongano isiyo ya lazima.
Pia, wameitaka serikali kusikiliza sauti za wananchi katika kila hatua ya kupanga na kutekeleza miradi ya maendeleo, wakisisitiza kuwa maendeleo ya kweli hayawezi kufikiwa bila ushirikishwaji wa wananchi.
Zaidi ya hayo, wameitaka serikali kutowachukulia wanaharakati kama wahalifu, bali kutofautisha wazi kati ya wale wanaovunja sheria na wale wanaotekeleza wajibu wao wa kikatiba wa kushiriki katika ujenzi wa taifa.
Mkutano huo umetajwa kuwa hatua muhimu ya kujenga maelewano na kuimarisha demokrasia ya ushirikishwaji katika kaunti ya Kajiado.