

By Felix Wanjala.
Viongozi kadhaa kutoka eneo la Magharibi wameendelea kuelekeza lawama kwa serikali, wakimtaka Rais William Ruto kusitisha mkataba kati ya serikali na mwekezaji Jaswant Rai unaohusu upangaji wa kiwanda cha sukari cha Nzoia.
Licha ya hayo, Naibu Rais Kithure Kindiki ametetea mageuzi yanayoendelea katika sekta ya kilimo, akisema ni sehemu ya juhudi za kuinua uchumi wa taifa. Alitoa kauli hiyo alipokutana na maafisa wakuu wa Wizara ya Kilimo katika makazi yake rasmi ya Karen, Nairobi.
Wabunge kutoka eneo hilo wamesisitiza kuwa mchakato wa upangaji wa viwanda hivyo haukuhusisha maoni ya wananchi wala viongozi wa eneo husika. Wamemtaka Rais Ruto atangulize utekelezaji wa ahadi alizowapa wakazi wa Magharibi kabla ya kuendeleza mipango mingine ya maendeleo.

Katika kampeni za uchaguzi, Rais Ruto aliahidi kushirikiana na viongozi wa Magharibi wakiongozwa na Musalia Mudavadi (Mkuu wa Mawaziri) na Moses Wetangโula (Spika wa Bunge la Kitaifa) kuhakikisha eneo hilo linapata asilimia 30 ya nafasi katika serikali.
Ahadi hizi zilijumuisha utoaji wa nafasi muhimu serikalini, ikiwemo nafasi sita za uwaziri, ufufuzi wa kiwanda cha sukari cha Nzoia kwa kuleta mitambo mipya ndani ya siku 100 za kwanza, na ujenzi wa zaidi ya kilomita 1,000 za barabara mpya pamoja na kukamilisha zile zilizokwama.
Hata hivyo, utekelezaji wa baadhi ya ahadi hizo umeonekana kuwa wa polepole, hali ambayo imezua maswali na kuibua shinikizo kutoka kwa viongozi wa eneo hilo kuhusu kujitolea kwa serikali katika kutimiza matarajio ya wananchi.
Viongozi hao sasa wanatoa wito kwa serikali kushughulikia kwa dharura changamoto zinazokwamisha utekelezaji wa ahadi hizo, wakisisitiza kuwa maendeleo ya eneo la Magharibi hayawezi kufanikishwa bila ushirikiano wa kweli, usawa katika ugavi wa rasilimali, na kuheshimu makubaliano ya awali.

Wanahimiza Rais Ruto kufungua mazungumzo ya wazi na viongozi wa eneo hilo ili kurejesha imani ya wananchi na kuhakikisha kuwa kila sehemu ya nchi inanufaika na matunda ya utawala wa sasa.
Viongozi hao wamesisitiza kuwa utekelezaji wa ahadi zilizotolewa kwa wakazi wa Magharibi si jambo la hiari bali ni deni la kisiasa linalopaswa kulipwa. Wameonya kuwa endapo serikali haitachukua hatua madhubuti na za haraka, basi huenda wakaazi wa eneo hilo wakapoteza imani na utawala wa sasa.
Wametaka serikali kuacha siasa za porojo na kuanza kutekeleza miradi iliyoahidiwa ili kuhakikisha maendeleo ya kweli yanawafikia wananchi wa kawaida. Kwa sasa, macho yote yako kwa Rais Ruto kuona iwapo atajibu wito huo kwa hatua za maana.
