

BY ALEX WEKESA.
Mbunge wa Bumula, Jack Wanami Wamboka, amemhimiza Rais William Ruto kuchukua hatua kali dhidi ya viongozi wa serikali wanaoshindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo, akisema wanaongeza mzigo kwa Rais.
Katika hafla ya uzinduzi wa mradi wa kuwasaidia akina mama wa mboga katika eneo bunge lake, Wamboka alionesha wasiwasi kuhusu uwajibikaji wa baadhi ya maafisa wa serikali, akirejelea kisa cha mauaji ya mwanablogu Mwalimu Albert Ojwang’, ambapo kulikuwa na madai kwamba makundi fulani yanahusika.
Wamboka, ambaye ni mbunge wa chama cha DAP-K, alikosoa serikali ya Kenya Kwanza kwa kushindwa kutimiza ahadi ambazo Rais Ruto alizitoa wakati wa kampeni za 2022. Alielezea kutoridhika na jinsi idadi kubwa ya vijana katika eneo bunge la Bumula wanavyokosa nafasi za ajira licha ya ahadi za kuwaajiri katika idara za jeshi na polisi.

Alihimiza serikali kubuni nafasi nyingi za ajira ili kusaidia vijana kujikimu kimaisha.Aidha, Wamboka alitoa onyo kwa Spika wa Bunge la Kitaifa, Moses Wetang’ula, na Waziri Musalia Mudavadi, kuhusu jinsi wanavyoshughulikia viongozi wachanga kwenye ulingo wa kisiasa. Aliwataka viongozi hao kuwasikiliza na kuwasaidia vijana kutoka eneo la mkoa wa magharibi, hasa Bungoma, katika kupigania nafasi zao ndani ya serikali na kutetea maslahi ya wananchi wa kawaida.”Wachana na Wamboka, Majimbo Kalasinga, Natembeya, na Edwin Sifuna, kama kweli ni viongozi, jitokezeni mtetea sauti ya watu,” Wamboka alisema, akisisitiza umuhimu wa kushirikiana na vijana katika uongozi.
Alimalizia kwa kuwataka wakaazi wa Bumula kumuunga mkono katika uchaguzi mkuu wa 2027 ili kuweza kuboresha maisha ya wapiga kura wake na kupambana na umaskini.