

Daktari Juma Mukwana ameisifu timu ya taifa ya soka, Harambee Stars, kwa kuonesha ari, bidii na ujasiri mkubwa tangu kuanza kwa mashindano ya CHAN. Akizungumza kwa furaha, Dkt. Mukwana alieleza kuwa vijana hao wamechangia pakubwa katika kuimarisha mshikamano wa kitaifa kupitia mchezo wa soka.
Katika hotuba yake, Dkt. Mukwana alitumia fursa hiyo kumshukuru Rais William Ruto kwa juhudi zake za dhati katika kukuza vipaji vya vijana, hasa kupitia uboreshaji wa miundombinu ya michezo. Alibainisha kuwa tangu mwaka 1987, chini ya utawala wa Rais wa zamani Daniel Arap Moi, hakukuwa na ujenzi mpya wa viwanja vya michezo hadi Rais Ruto alipochukua hatamu za uongozi.“Rais Ruto ameonesha kujitolea kwa hali ya juu. Amejenga uwanja wa Kasarani kwa viwango vya kimataifa, amekarabati uwanja wa Nyayo, na pia kuna maendeleo makubwa katika viwanja vya Talanta, Kanduyi, Homa Bay na Machakos,” alisema Dkt. Mukwana.

Aidha, aliwahimiza Wakenya kuendelea kuwaunga mkono wachezaji wa nyumbani badala ya kuelekeza mapenzi yao kwa timu za kigeni kama Chelsea na Arsenal. Alisisitiza kuwa iwapo timu za taifa zitaungwa mkono kwa malipo stahiki na mazingira bora ya kufanyia mazoezi na kucheza, zina uwezo wa kufikia viwango vya juu kimataifa.Dkt. Mukwana alihitimisha kwa kuwataka Wakenya kuendeleza moyo wa uzalendo na kuwekeza kwa dhati katika timu za nyumbani ili kuinua sekta ya michezo nchini.