 
                
BY FELIX WANJALA.
Mgombea wa ugavana wa Bungoma, Timothy Wanyonyi, ameungana na Wakenya kuomboleza kifo cha kiongozi wa upinzani Hayati Raila Odinga, akimsifu kama kiongozi wa kawaida aliyekuwa karibu na kila mtu kutoka kwa viongozi wa kitaifa hadi kwa mwananchi wa kawaida.
Katika risala yake ya rambirambi, Wanyonyi alisimulia kwa hisia jinsi alivyokutana na Raila kwa mara ya kwanza, akimtaja kama mtu mwenye moyo wa utu na msimamo wa kisiasa unaoangazia maslahi ya taifa. Alikumbuka jinsi Raila alimuunga mkono Hayati Mwai Kibaki katika uchaguzi wa 2002, akionyesha uzalendo wa hali ya juu.

Wanyonyi pia alitaja safari ndefu ya Raila katika kuwania urais,kuanzia mwaka wa 1997 hadi 2022,akisema kuwa alikuwa na ufuasi wa kipekee na wa kuigwa. “Alikuwa mfano wa kiongozi anayesimama kwa haki, demokrasia, na katiba,” alisema.Raila ametajwa na Wanyonyi kama mtetezi mkuu wa katiba, baba wa demokrasia, na mwasisi wa serikali za ugatuzi, mchango ambao umeacha alama isiyofutika katika historia ya Kenya.Wakaazi wa Bungoma pia walitoa ushuhuda wao, wakimkumbuka Raila kama kiongozi wa kitaifa aliyegusa maisha ya wengi na kuacha urithi wa kisiasa unaoenziwa na vizazi vijavyo.
 
                 
                 
                 
                 
                