BY VIONA SIMIYU

Polisi mjini Eldoret, Kaunti ya Uasin Gishu, wamefanikiwa kuzima jaribio la ujambazi wa kutumia silaha baada ya kuwaua kwa risasi washukiwa wanne katika makabiliano ya alfajiri yaliyotokea kwenye barabara ya Eldoret–Kiplombe.
Tukio hilo lilitokea majira ya saa sita usiku karibu na makutano ya Greenfield Junction.Kwa mujibu wa polisi, maafisa walikuwa wakitekeleza operesheni ya kijasusi baada ya kupokea taarifa kuhusu kundi la wahalifu waliokuwa wakiwahangaisha wakazi na wasafiri katika eneo hilo.Maafisa hao walifika eneo la tukio na kuwakuta washukiwa sita wakiwa wamevalia mavazi yanayofanana na ya kijeshi huku wakiwapora wananchi.Polisi wanasema walipojitambulisha na kuwaamuru washukiwa wajisalimishe, kundi hilo lilifungua moto dhidi ya maafisa. Hali hiyo ilisababisha majibizano makali ya risasi kati ya pande hizo.Katika makabiliano hayo, washukiwa wanne walipigwa risasi na kufariki papo hapo, huku wengine wawili wakitoroka wakiwa na majeraha ya risasi.
Polisi wameanzisha msako mkali wa kuwatafuta washukiwa hao waliotoroka.Maafisa wa usalama wanaamini kundi hilo linahusishwa na msururu wa matukio ya ujambazi wa kutumia silaha yaliyoshuhudiwa katika maeneo ya Kitale, Kapenguria, Nandi, Marakwet na Eldoret katika miezi ya hivi karibuni.Baada ya upekuzi katika eneo la tukio, polisi walipata bastola iliyokuwa imejaa risasi, vifaa vinavyodaiwa kutumika kuvunja nyumba na biashara, simu kadhaa za mkononi pamoja na kamba zinazoshukiwa kutumika kuwafunga wahanga wa ujambazi.Miili ya washukiwa hao imehamishwa hadi katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Rufaa na Mafunzo ya Moi (MTRH), huku uchunguzi ukiendelea kubaini utambulisho wao na iwapo walihusika katika matukio mengine ya uhalifu.Polisi wamesema uchunguzi wa kina unaendelea na kwamba vielelezo vilivyopatikana vitachunguzwa ili kusaidia kuwatambua washirika wengine wa genge hilo na kufanikisha msako dhidi ya waliotoroka.

Wakazi wa Eldoret wamepongeza hatua ya polisi ya kuingilia kati kwa haraka, wakisema matukio ya ujambazi yamekuwa yakizua hofu hasa nyakati za usiku. Hata hivyo, wametoa wito kwa vyombo vya usalama kuimarisha doria ili kuzuia visa kama hivyo kutokea tena.Polisi sasa wanawasihi wananchi wenye taarifa zozote kuhusu washukiwa waliotoroka kujitokeza na kushirikiana na vyombo vya usalama, wakisisitiza kuwa operesheni dhidi ya makundi ya wahalifu itaendelea hadi wote wanaohusishwa na uhalifu huo wakamatwe.