BY GELAS SITUMA

Chama cha ODM kimesema kitamtangaza rasmi mgombea wa urais atakayekiunga mkono 2027 kabla ya mwezi Desemba mwaka huu.Akizungumza Nyanza wakati wa mkutano wa mashauriano na wafuasi, Mwenyekiti Oburu Odinga alisema uamuzi huo utatokana na maoni ya wanachama kote nchini. “Tunataka mgombea wetu awe mtu aliyechaguliwa na wanachama, sio kuamuliwa ofisini. Ndiyo maana tunasikiza ground kwanza,” alisema Odinga.
Viongozi wa ODM pia waliwasha kampeni ya usajili wa wapiga kura. Waliwataka wakazi wa Nyanza hasa vijana kujipatia vitambulisho na kujisajili IEBC ikianza zoezi hilo. “Kura nyingi ndizo silaha yetu 2027. Tusipojiandikisha tutalia baadaye,” aliongeza mmoja wa viongozi.Katika mkutano huo huo, Waziri wa Nishati Opiyo Wandayi na Dkt. Raymond Omollo wa Usalama wa Ndani walitangaza kuunga mkono Rais William Ruto kuwania muhula wa pili.
“Kenya Kwanza imeanza miradi mikubwa. Tunahitaji miaka 5 nyingine ili tuikamilishe,” walisema.Viongozi hao pia walikosoa siasa za migawanyiko na kusema taifa linahitaji umoja ili miradi ya maendeleo ifanikiwe.Tangazo la ODM linakuja wakati siasa za 2027 zikianza kupamba moto. Rais Ruto tayari anatarajiwa kutetea kiti chake, huku wagombea wengine wakijiandaa kujiingiza kwenye kinyang’anyiro.