BY CYNTHIA ELIZABETH

Zaidi ya muongo mmoja uliopita, Wakenya walipiga kura kuidhinisha Katiba Mpya iliyoleta mfumo wa ugatuzi. Lengo kuu lilikuwa kusogeza huduma za kimsingi karibu na wananchi, hasa sekta ya afya ambayo kwa miaka mingi ilikuwa ikiongozwa kutoka makuu jijini Nairobi.
Tangu wakati huo, mabilioni ya shilingi yameelekezwa kwenye kaunti mbalimbali nchini. Hata hivyo, katika vijiji vya Kaunti ya Bungoma, swali kuu linalosalia miongoni mwa wakazi ni je, mabilioni hayo yanatafsiriwa kuwa huduma bora kwa mwananchi wa kawaida?Uchunguzi wetu katika vituo vya afya vya mashambani kama vile Ndalu, Makutano, na Kituo cha Mfano cha Tongaren unaonesha taswira ya kipekee.
Ni taswira inayodhihirisha jinsi maendeleo ya kimuundo yanavyokumbana na changamoto za uhalisia wa kifedha, mabadiliko ya sera za kitaifa, na wakati mwingine, michezo ya ndani ya mifumo ya afya.Katika mipango ya sasa ya kifedha, Idara ya Afya katika Kaunti ya Bungoma inapokea fungu kubwa zaidi la shilingi bilioni nne kutoka kwa jumla ya bajeti ya kaunti ya shilingi bilioni kumi na tano. Kwa macho ya kawaida, hili ni fungu kubwa linaloweza kubadilisha sura ya matibabu.
Lakini ukiingia ndani ya mtiririko wa pesa hizo, ukweli mchungu unaanza kujitokeza.Wachambuzi wa bajeti wanaeleza kuwa muundo wa matumizi ya fedha unaziacha kaunti zikiwa zimeshikwa koo. Bwana George, ambaye ni mchambuzi wa mifumo ya kifedha na bajeti, anafafanua kuwa mishahara pekee ya wafanyakazi wa afya inameza takriban shilingi bilioni tatu nukta saba kila mwaka.Ukiondoa mishahara hiyo kwenye lile fungu la bilioni nne, kaunti inabaki na shilingi milioni mia nne tu kwa ajili ya uendeshaji wa vituo vyote,” anafafanua Bwana George. “Hali hii inamaanisha kuwa serikali ya kaunti inaweza kuwa na uwezo wa kujenga majengo mazuri ya zahanati, lakini inakosa fedha za kununua vifaa vya kisasa vya matibabu, kuweka dawa, au kugharamia mafuta ya magari ya wagonjwa.
Wataalamu wengi wananyoshea kidole fomula ya kitaifa ya ugawaji wa mapato. Wakati kaunti zikibeba mzigo mzito wa kutoa huduma za matibabu kila siku, asilimia sabini na tano ya mapato yote ya nchi inabaki mikononi mwa serikali kuu kule Nairobi, huku kaunti zikiambulia asilimia kumi na tano pekee.Matokeo ya uhaba huu wa fedha za uendeshaji yanaonekana wazi kwenye madirisha ya kutoa dawa katika vituo vya mashambani.
Wagonjwa wanaotembelea vituo kama Ndalu au Makutano mara kwa mara huondoka wakiwa wamesika vyeti tupu vya daktari, huku wakiombwa kununua dawa muhimu kwa pesa zao wenyewe kutoka kwenye maduka ya kibinafsi yaliyo nje ya lango la hospitali.Hata hivyo, uchunguzi wetu unaonesha kuwa uhaba wa fedha sio sababu pekee. Wadokezi wa ndani ndani ya mfumo wa afya wanafichua uwepo wa mchezo mchafu unaotajwa na wengi kama ukora wa kitabibu.

Baadhi ya madaktari walioajiriwa na serikali wanamiliki maduka ya dawa au kliniki za kibinafsi kando na kazi zao za umma. Ili kufanikisha biashara zao, baadhi yao wanadai kimakusudi kuwa hospitali haina dawa ili kuwaelekeza wagonjwa maskini kwenye maduka yao ya nje ili wajinufaishe kifedha.
Vituo vya afya vya mashambani vinapokosa madaktari wa kutosha au vifaa vya vipimo kama mashine za Xray, athari yake inasababisha mtiririko mkubwa wa wagonjwa kuelekea Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Bungoma (BCRH). Hali hii imesababisha uvumi mwingi miongoni mwa jamii, ikiwemo madai kuwa hospitali hiyo imelemewa kiasi cha wagonjwa kulala wawili kwenye kitanda kimoja.Utawala wa hospitali hiyo kuu hata hivyo unakanusha vikali madai hayo.
Gloria Situma, ambaye ni Afisa wa Mawasiliano katika Hospitali ya Rufaa ya Bungoma, anakiri kuwa kuna idadi kubwa sana ya wagonjwa wanaotumwa hapo, lakini anasisitiza kuwa uvumi wa kushiriki vitanda si wa kweli.Kuna msongamano kwa sababu kituo hiki kinapokea wagonjwa wengi kutoka kote kaunti kutokana na uwepo wa vitengo maalum kama kile cha kusafisha figo,” anasema Gloria Situma. “Hospitali haishawishi wala kuruhusu wagonjwa kulala wawili kwenye kitanda kimoja.
Tumeongeza vitanda na magodoro kati ya sabini na mia moja hivi majuzi, na tunatumia madaktari walio kwenye mafunzo pamoja na wauguzi wa mikataba ya muda ili kudhibiti mzigo wa kazi.”Wakati hospitali ikipambana na changamoto hizo za ndani, mfumo mpya wa kitaifa wa Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA) umerundika daraja jipya la mabadiliko ya kiutawala. Lengo la SHA ni kuhakikisha kila mwananchi anapata matibabu bila kuumia kifedha, lakini kwenye madawati ya malipo, mabadiliko haya yameleta vikwazo vya kiteknolojia.
Charleen Makungu Mbone, ambaye anasimamia kitengo cha malipo ya SHA katika Hospitali ya Rufaa ya Bungoma, anaeleza kuwa ingawa mfumo wenyewe umeundwa vizuri ili kusaidia wagonjwa, changamoto za kukatika kwa mtandao na mifumo ya kielektroniki mara kwa mara zinasababisha ucheleweshaji mkubwa wakati wa kuthibiti data za wagonjwa kabla hawajaruhusiwa kupata huduma.Mbali na changamoto za kimtandao, mfumo huu unakumbana na kizuizi cha kijamii. Ili kusajiliwa kwenye mfumo wa kidijitali wa SHA, mwananchi anahitajika kuwa na kitambulisho cha kitaifa. Katika maeneo mengi ya vijijini kaunti ya Bungoma, idadi kubwa ya wazee wasiojiweza hawana hati hizi muhimu.

Matokeo yake, wazee hawa wanajikuta wamefungiwa nje ya mfumo wa SHA, hali inayowalazimu kulipia matibabu kwa pesa taslimu kutoka mifukoni mwao, jambo linalopingana na malengo makuu ya afya kwa wote.Sekta ya dharura na uokoaji pia inashuhudia changamoto sawa za mpito.Chini ya mwongozo wa kitaifa wa SHA, kuna mpango wa kuanzisha mfumo wa kisasa wa kidijitali uitwao u-dial kwa ajili ya kuratibu na kuitisha magari ya wagonjwa yaani ambulensi nchi nzima.
Hata hivyo, wachambuzi wa mifumo wanaonesha kuwa mfumo huo bado haujaanza kufanya kazi kwa manufaa ya mwananchi wa kawaida wa Bungoma, huku kukiwa na malalamiko kuhusu magari mengi ya wagonjwa kusimama yakiwa yameharibika au kukosa ukarabati.Lakini kwa upande mwingine, maandalizi ya ndani yanaonesha matumaini.
Charleen Makungu Mbone anathibitisha kuwa hospitali ya rufaa imeshaanza kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wake kuhusu utaratibu huo mpya wa kidijitali.Wafanyakazi wa utawala wanajifunza jinsi ya kufuatilia kesi za dharura kwa njia ya kielektroniki ili mfumo huo utakapozinduliwa kikamilifu uweze kupokea wagonjwa bila kuchelewa.Ugatuzi wa afya uliahidi kufanya matibabu kuwa haki inayopatikana kwa urahisi karibu na nyumba ya kila mwananchi maskini mashambani, huku mfumo mpya wa SHA ukilenga kuondoa mzigo wa gharama.
Hata hivyo, wakati uhalisia wa shilingi milioni mia nne za uendeshaji katika Kaunti ya Bungoma unapokabiliana na changamoto za mifumo ya kidijitali, ukosefu wa vitambulisho kwa wazee, na michezo ya siri ya kimaslahi, mtihani mkuu unabaki pale pale.Ufanisi wa afya katika kaunti hautapimwa kwa mabilioni ya shilingi yanayotangazwa kwenye kumbi za bunge la kaunti, bali utapimwa kwa uwezo wa mwananchi wa kawaida wa Tongaren, Ndalu, au Makutano kupata vipimo vya maabara, dawa za kutosha, au gari la dharura la wagonjwa pale maisha yake yanapokuwa hatarini.