Huko Gaza, takriban watu 12 wakiwemo kinamama na watoto wameuawa walipokuwa katika msafara wa kuondoka Gaza Kaskazini kuelekea Kusini kufuatia shambulizi lililofanywa na Israel. Wapalestina hao walikuwa wakihama eneo hilo kutekeleza agizo la jeshi la Israel lililowataka wananchi kuondoka Kaskazini mwa Gaza kwa kile kilichadaiwa kwamba huenda jeshi hilo lingeshambulia eneo hilo. Kufuatia tukio hilo taarifa ziliibuka kwa mara ya kwanza jana jioni za mgomo wa msafara wa magari yanayoelekea Kusini mwa Gaza.
Kwa mujibu wa BBC, mgomo huo ulitokea katika mtaa wa Salah-al-Din moja ya njia mbili ambazo Wapalestina walioko Gaza Kaskazini hutumia kueleka Kusini mwa Gaza. Barabara hiyo ilijaa msongamano wa magari siku nzima jana huku wakazi wa Gaza walioko Kaskazini wakizingatia maonyo ya Israel ya kutaka kuondoka eneo hilo. BBC imeongeza kuwa wengi wa waliouawa ni wanawake na watoto ambao baadhi yao wanaonekana kuwa na umri wa miaka miwili hadi mitano. Wengi wanaonekana wamelala nyuma ya lori huku wengine wametawanyika kuzunguka barabara.
Magari mengine yaliyoharibika pia yameonekana kujaa katika eneo hilo. Wizara ya Afya ya Palestina inasema watu 70 waliuawa katika eneo la tukio, na imeilaumu Israel kwa shambulio hilo. Hata hivyo jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) limesema kuwa linachunguza lakini likasema maadui wake wanajaribu kuzuia raia kuondoka Kaskazini mwa Gaza. Zaidi ya watu 1,300 wameuawa nchini Israel wikendi iliyopita wakati wapiganaji wa Hamas walipovuka mpaka kushambulia raia na wanajeshi huku watu 2,200 wakiuawa katika kampeni ya Israel ya kulipua mabomu katika Ukanda wa Gaza iliyozinduliwa baada ya tukio hilo, mamlaka ya Palestina imesema.