
TANDAO MEDIA_ An image showing the Deputy President of Kenya, Professor Kithure Kindiki.

BRIGID SIKUKU.
Katika hali ya sasa ambapo ukosefu wa ajira unaendelea kuwa changamoto kubwa kwa vijana nchini, Kauli ya Naibu Rais Kithure Kindiki imezua hisia mseto. Akizungumza katika hafla ya vijana mjini Kitale kaunti ya Trans nzoia, Kindiki aliwataka vijana kuwasilisha maoni yao kwa njia mwafaka, ili kusaidia serikali kubuni nafasi za ajira mtandaoni, mitaani na hata nje ya nchi.
Naibu Rais alisisitiza kuwa serikali imeweka mikakati ya kipekee ya kusaidia vijana kupitia fursa zinazopatikana katika teknolojia, ubunifu na sekta za kimataifa. Alisema kuwa kwa kushirikiana na mashirika ya kibinafsi, serikali inalenga kufungua milango ya ajira kwa vijana waliokosa nafasi za kazi kwa muda mrefu.
Kwa mujibu wa Kindiki, vijana wanaweza kupata ajira kupitia majukwaa ya kidijitali kama vile kazi za mtandaoni, usafirishaji, huduma za kijamii na hata programu za kazi za muda nje ya nchi. Kauli hiyo imechukuliwa na baadhi kama matumaini mapya kwa kizazi kinachopambana na ukosefu wa ajira.
Hata hivyo, baadhi ya wananchi wamepinga kauli hiyo, wakisema kuwa ni porojo za kisiasa zisizo na msingi. Wanaamini kuwa serikali haijachukua hatua madhubuti kushughulikia ukosefu wa ajira, na badala yake inaendelea kutoa ahadi zisizotekelezeka.
Ni maneno tu kila mara. Vijana wamechoka kusikia mipango ambayo haionekani ikitekelezwa. “Tunahitaji vitendo, si ahadi mpya kila mwezi,” anasema Amos Wekesa, kijana mkazi wa Bungoma. Anadai kuwa licha ya kuhitimu chuoni miaka mitatu iliyopita, bado hajapata kazi.

Joseph Sifuna, anasema kuwa serikali haijawahi kuwafikia vijana mashinani. “Wanaongea kuhusu kazi mitandaoni, lakini vijijini hakuna hata intaneti ya kutosha. Wanahakikisha wanalenga mijini tu, wakitusahau sisi wengine,” anahoji kwa uchungu.
Ripoti za hivi karibuni zinaonyesha kuwa zaidi ya vijana nchini hawana ajira rasmi. Wataalamu wanakosoa serikali kwa kutotilia maanani miundombinu, mafunzo ya stadi za kazi, na uwezeshaji wa kijamii, kama njia muafaka ya kutatua tatizo hilo.
Ingawa kauli ya Naibu Rais inalenga kutia matumaini, ukweli unabaki kuwa vijana wengi wanahisi kusahaulika na kuachwa nyuma. Wito kutoka kwa wananchi ni kwamba serikali ianze kutekeleza kwa dhati sera za ajira, badala ya kuendelea kutoa ahadi zisizoambatana na hali halisi ya maisha ya vijana wengi wa Kenya