

FELIX WANJALA.
Wakizungumza wakati wa maadhimisho ya miaka 60 ya huduma ya Mtawa Margret katika Parokia ya Kanisa Katoliki la Misikhu, viongozi mbalimbali wakiongozwa na Mbunge wa Westlands, Tim Wanyonyi, walitoa wito wa heshima na usawa katika siasa.
Viongozi hao walilaani baadhi ya wapinzani wao kwa kile walichokitaja kuwa ni dharau dhidi ya watu wenye ulemavu wakati wa hafla za kisiasa, wakisisitiza kuwa kila Mkenya anastahili kuheshimiwa bila kujali hali yake ya kiafya au kimwili.Mbunge Wanyonyi, ambaye ametangaza nia ya kuwania kiti cha Ugavana katika Kaunti ya Bungoma, aliwahimiza wakazi wa kaunti hiyo kumwunga mkono, akitaja rekodi yake ya maendeleo katika eneo bunge la Westlands kama ushahidi wa uwezo wake wa uongozi.
Aidha, viongozi wengine waliokuwa ameandamana nao, wakiwemo wawakilishi wa wadi, walielezea kuunga mkono kwao azma ya Wanyonyi, wakiahidi kushirikiana naye katika kuleta maendeleo kwa kaunti hiyo.
Katika hotuba yake, Wanyonyi aliahidi kwamba iwapo atachaguliwa kuwa Gavana wa Bungoma, ataweka kipaumbele katika kuboresha sekta za elimu, afya na kilimo. Pia aliahidi kubuni nafasi za ajira, kuimarisha miundombinu na kuhakikisha usambazaji wa rasilimali unafanyika kwa usawa katika maeneo yote ya kaunti.