
Former Deputy President Rigathi Gachagua giving a press conference in Bogota, Colombia on September 12, 2023. (Photo by Sebastian Barros via Getty Images)

BY BRIGID SIKUKU.
Aliyekuwa Naibu Rais na Kiongozi wa chama cha DCP, Rigathi Gachagua, ametangaza rasmi nia yake ya kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2027. Taarifa hiyo imeibua mjadala mkubwa kote nchini, huku mitazamo tofauti ikijitokeza kuhusu uwezo wake wa kuongoza taifa hili katika kipindi kijacho.
Akizungumza katika mkutano wa vijana uliofanyika jijini Nairobi, Gachagua alisema kuwa serikali yake itajikita katika kupambana na ufisadi, kuimarisha mifumo ya uwajibikaji serikalini, na kuhakikisha kuwa kila mwananchi anapata nafasi sawa ya kufaidika na rasilimali za taifa. “Nitakomesha ufisadi, na nitahakikisha viongozi wote wanawajibika kwa kila hatua wanayochukua,” alisisitiza.Tangazo hilo limepokelewa kwa mitazamo tofauti kutoka kwa wananchi.
Wapo wanaoamini kuwa Gachagua amejitokeza kwa ujasiri kuonyesha dhamira ya kulitumikia taifa, na wanamtazama kama kiongozi anayeweza kuleta mabadiliko makubwa kwa kutumia uzoefu wake serikalini. “Tunataka viongozi wasioogopa kusema ukweli, na Gachagua anaonekana kujitokeza kwa hilo,” alisema Husein Abdul, mkaazi wa Nairobi.Hata hivyo, kuna wengine wanaotilia shaka uwezo wa Gachagua kuongoza nchi katika misingi ya umoja wa kitaifa na utawala bora.
Wengine wamedokeza kuwa kauli zake za awali na mtindo wake wa uongozi huenda usiwavutie wapiga kura wote. “Binafsi bado sijaona dira pana kutoka kwake kuhusu masuala ya elimu, afya na mshikamano wa kitaifa,” alisema Enos Wekesa, kijana kutoka Bungoma.Jorom Siremi, mkaazi mwingine, alisema kuwa Gachagua anapaswa kutumia nafasi hii kuzungumza moja kwa moja na wananchi katika maeneo ya mashinani ili kueleza maono yake kwa kina. “Sio tu kutangaza, tunataka kuona hatua mipango ya vitendo itakayoathiri maisha yetu moja kwa moja,” alieleza.
Kwa sasa, Gachagua ameanza kujipanga kwa mikutano ya kisiasa katika maeneo mbalimbali nchini ili kuimarisha ushawishi wake, huku akisisitiza kuwa safari yake ya kisiasa itajengwa juu ya maadili, uwazi na kuondoa siasa za matusi. Tangazo lake linakuja wakati siasa za 2027 zikianza kuchukua mwelekeo wa mapema.Wachambuzi wa siasa wanasema kuwa kuwania kwa Gachagua kunaleta mvuto mpya katika kinyang’anyiro cha urais, hasa ikizingatiwa kuwa huenda akawa mpinzani wa aliyekuwa mshirika wake wa karibu Rais William Ruto iwapo kutakuwa na mvutano wa kisera au wa ndani ya miungano ya kisiasa.
Kwa ujumla, tangazo la Rigathi Gachagua limefungua ukurasa mpya wa siasa za uchaguzi wa 2027. Wakati baadhi ya wananchi wakiweka matumaini yao kwake, wengine wanasubiri kwa tahadhari kuona iwapo atatoa dira ya kweli itakayojibu maswali ya wananchi kuhusu uchumi na umoja wa kitaifa.