

BY BRIGID SIKUKU.
Wazazi nchini wameiomba serikali kuharakisha ulipaji wa deni la zaidi ya shilingi bilioni tatu kwa wachapishaji wa vitabu, wakionya kuwa ucheleweshaji wa malipo hayo unaweza kuhujumu maandalizi ya wanafunzi wa Gredi ya Tisa wanaotarajiwa kujiunga na Kidato cha Kwanza mwaka ujao.
Kwa mujibu wa wazazi, ukosefu wa vitabu muhimu vya kiada unaweza kuwa kikwazo kikubwa kwa mafanikio ya mfumo mpya wa elimu ya Mtaala wa Umahiri (CBC), hasa kwa wanafunzi wanaotarajiwa kufanya mpito huo kwa mara ya kwanza.Wachapishaji nao wamelalamikia kucheleweshwa kwa malipo, wakisema kuwa hali hiyo inawalemaza kifedha na kuwafanya washindwe kuchapisha vitabu vipya vinavyohitajika kwa mtaala wa CBC.
Wamefanya serikali bado haijalipa zaidi ya shilingi bilioni tatu, hali inayowatia wasiwasi kuhusu uwezo wa kutimiza mahitaji ya shule kwa wakati.Dennis Wekesa, mkaazi wa Bungoma na mzazi wa mtoto aliye Gredi ya Nane, anasema:”Tunawasiwasi watoto wetu wataingia Kidato cha Kwanza bila maandalizi ya kutosha. Serikali isafishe hali hii mapema,” amesema kwa tahadhari.Wizara ya Elimu hata hivyo imeendelea kusisitiza kuwa iko tayari kushughulikia mahitaji ya wanafunzi wote wanaotarajiwa kuingia Gredi ya Tisa, ikisema kuwa maandalizi ya kitaifa yanaendelea vyema na vifaa muhimu vitapatikana kwa wakati.
Ochieng Aput, anaunga mkono mtaala mpya lakini anahofia kuwa ukosefu wa vifaa utaharibu nia njema ya mfumo huo. “CBC ni mfumo mzuri, lakini bila vitabu na vifaa, watoto wetu watasalia nyuma,” amesema.Mpango wa Gredi ya Tisa unatarajiwa kuzingatia si tu mitihani, bali pia mwelekeo wa taaluma ya mwanafunzi, kulingana na vipawa na uwezo wao. Serikali inasema hii inalenga kuwajengea wanafunzi msingi bora wa maisha ya baadaye.Kwa jumla, zaidi ya wanafunzi milioni 1.2 wanatarajiwa kujiunga na Gredi ya Tisa mwaka ujao, huku serikali ikiahidi kuimarisha mazingira ya kujifunzia na kuhakikisha hakuna mwanafunzi anayeachwa nyuma.