

BY FELIX WANJALA.
Mwakilishi wa kike wa Kaunti ya Bungoma, Bi. Catherine Wambilianga, ameelezea masikitiko yake na kulaani vikali tukio la madai ya kubakwa kwa mwanafunzi wa kidato cha tatu katika hospitali moja ya kibinafsi mjini Bungoma.
Kwa sasa, familia ya mwanafunzi huyo inaendelea kusaka haki, ikisisitiza umuhimu wa kufanyika kwa uchunguzi wa kina na wa haki ili kuhakikisha ukweli unafichuliwa.
Mwanafunzi huyo, ambaye ana umri wa miaka kumi na minane, anaripotiwa kuwa alipitia unyanyasaji huo akiwa katika mazingira ambayo yalipaswa kuwa salama kwake.

Familia yake pia imetaja wasiwasi wake kuwa huenda kuna juhudi za kuficha au kuharibu ushahidi muhimu katika kesi hiyo.
Katika hatua nyingine, Kamanda wa Polisi wa eneo la Bungoma Kusini, Bw. William Letting, ameonya vikali kuwa yeyote atakayejihusisha na vitendo vya unyanyasaji dhidi ya wanafunzi atakumbana na hatua kali za kisheria, huku akisisitiza dhamira ya vyombo vya usalama kulinda haki na ustawi wa watoto na wanafunzi.