FILE-Spika wa bunge la kitaifa Moses Wetang'ula kwenye hafla fulani.PHOTO/TANDAO MEDIA/FILE

BY FELIX WANJALA.
Katika kipindi ambacho taifa linaendelea kushuhudia maandalizi ya viongozi kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027, sauti za kutaka jamii ya Magharibi kushikamana kwa ajili ya maendeleo zinazidi kupamba moto.
Wito huu unalenga kuimarisha mshikamano wa kikanda ili kuleta mabadiliko ya kijamii na kiuchumi kupitia ushirikiano wa kisiasa.Hata hivyo, ndoto ya umoja huo huenda ikakumbwa na changamoto kutokana na chaguzi ndogo zinazotarajiwa kufanyika katika maeneo kadhaa ya Magharibi, ikiwemo eneo bunge la Malava na wadi za Kisa Magharibi na Chwele Kabuchai.
Tayari kampeni zimeanza kushika kasi huku viongozi wakuu wakionekana kujitokeza kwa nguvu, kila mmoja akijaribu kujinadi na kuvutia uungwaji mkono.Majibizano ya kisiasa na mikwaruzano ya maneno imeanza kushamiri, hali inayoweza kudhoofisha juhudi za kuunganisha jamii hiyo.
Wakati huo huo, baadhi ya wadau wa kisiasa wanasisitiza kuwa Magharibi ni lazima iwe na nafasi ya kumrithi Rais William Ruto ifikapo uchaguzi wa 2032, wakidai kuwa idadi ya wapiga kura wa eneo hilo ni ya kutosha kuleta mabadiliko makubwa katika uongozi wa taifa.