Samson Cherargei, during a sitting on Thursday, February 12, 2026. PHOTO/@scherargei/X

BY FELIX WANJALA
Seneta wa Nandi, Samson Cherargei, ameibua mjadala mkali baada ya kudai kuwa chama cha Ford Kenya hakikuchangia lolote katika ushindi wa Rais William Ruto mwaka 2022. Akizungumza kwenye mahojiano na runinga moja humu nchini, Cherargei alisisitiza kuwa umaarufu wa Ruto binafsi ndio uliompa kura nyingi katika Kaunti ya Bungoma, na wala si juhudi za viongozi wa eneo hilo.
Kauli hii imeibuka siku moja tu baada ya Ford Kenya kumsuta Cherargei kwa madai yake ya kutaka chama hicho kivunjwe ili kushirikiana na UDA. Seneta huyo amerejea tena na kuongeza moto, akisisitiza kuwa kura za Bungoma zilikuwa matokeo ya ushawishi binafsi wa Rais Ruto, jambo linalopingwa vikali na wafuasi wa Ford Kenya.
Kwa mujibu wa rekodi za IEBC, Ruto alipata kura 255,755 Bungoma, akimshinda mpinzani wake wa wakati huo, Hayati Raila Odinga, aliyepata takribani kura 145,106. Hata hivyo, Ford Kenya ilijizolea nafasi nyingi za uongozi katika kaunti hiyo, ikiwemo wawakilishi wadi 20, wabunge 4, mwakilishi wa kike, seneta na gavana. UDA kwa upande wake ilipata wawakilishi wadi 9, huku DAP-K ikipata 10.

Spika wa Bunge la Taifa na kiongozi wa Ford Kenya, Moses Wetangula, mara kwa mara amesisitiza kuwa kura za Bungoma ndizo “ziliangusha ratili” na kumpa Ruto ushindi wa urais. Hivi karibuni, Rais Ruto ameonekana kuimarisha ngome yake Bungoma kwa kumteua Gavana Kenneth Lusaka kuwa mratibu mkuu wa kampeni zake, pamoja na kuunganisha wabunge wa eneo hilo chini ya mbunge wa Sirisia, John Waluke.
Cherargei anadai kuwa malumbano ya ndani ya Ford Kenya yanahujumu juhudi za Rais Ruto kudumisha ushawishi wake katika eneo hilo. Kwa mtazamo wake, iwapo Ford Kenya itavunjwa, viongozi wa Bungoma wataweza kwa urahisi kuwarai wananchi kuunga mkono chama cha UDA.