President William Ruto with ODM Party Leader Oburu Oginga on Friday, March 20, 2026,during an Eid-ul-Fitr luncheon at Kisumu State Lodge. Photo/Courtesy

BY FELIX WANJALA
Rais William Ruto ameongoza taifa pamoja na jamii ya Waislamu kusherehekea sherehe ya Idd-ul-Fitr katika Ikulu ndogo ya Kisumu. Sherehe hizo ziliambatana na wito wa mshikamano wa kitaifa, huku baadhi ya waumini wakimtaka rais kutuliza joto la kisiasa ambalo wanasema limeanza kupanda hata kabla ya uchaguzi mkuu ujao.
Akihutubia viongozi na waumini, Rais Ruto alisisitiza kuwa ushirikiano wake na chama cha ODM utachochea umoja nchini. Aliwahimiza viongozi na wananchi kuonyesha upendo kwa wengine kama njia ya kujenga taifa lenye mshikamano. Viongozi aliokuwa ameandamana nao, akiwemo kiongozi wa ODM Oburu Oginga, waliahidi kuendelea kushirikiana na serikali kwa manufaa ya maendeleo ya eneo hilo.
Wakati huo huo, waumini wa Kiislamu kutoka zaidi ya misikiti ishirini mjini Bungoma walikusanyika katika Bungoma Muslim Centre kusherehekea kukamilika kwa mwezi mtukufu wa Ramadhan. Walitoa wito kwa viongozi kujitenga na matamshi yanayoweza kuchochea uhasama wa kijamii. Aidha, walilaani mapigano yanayoendelea Mashariki ya Kati, wakishtumu mataifa ya Israel na Marekani kwa madai ya kuendeleza hujuma dhidi ya wananchi wa Iran.