Katibu Mkuu wa chama cha Ford Kenya, John Chikati. PICHA/KWA HISANI/
BY FELIX WANJALA

Katibu Mkuu wa chama cha Ford Kenya, John Chikati, ameibua mjadala moto baada ya kuwasuta vikali baadhi ya viongozi wanaotaka chama hicho kivunjwe ili kishirikiane kikamilifu na serikali. Chikati amesisitiza kuwa Ford Kenya, kama chama tanzu cha muungano wa Kenya Kwanza, kitaendelea kushirikiana bila kuvunjwa. Kauli yake imezua maoni tofauti miongoni mwa wananchi.
Shinikizo kutoka kwa baadhi ya viongozi wa UDA kumtaka kiongozi wa Ford Kenya, Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetangula, kukivunja chama cha Simba, limeendelea kuwakera wanachama wa Ford Kenya. Chikati amesisitiza kuwa chama hicho kilichangia pakubwa ushindi wa Rais William Ruto katika uchaguzi wa 2022, na hivyo hakina sababu ya kuvunjwa.
Wananchi wamegawanyika kuhusu suala hili baadhi wanadai ni wakati muafaka kwa eneo la Magharibi kuunga mkono chama kipya kitakachoanzishwa na viongozi chipukizi wenye maono ya mageuzi.Wengine wanahisi Ford Kenya imekuwa “meli ya kisiasa” ya Magharibi kwa muda mrefu, na kuvunjwa kwake kutapunguza umaarufu wa eneo hilo katika siasa za kitaifa.
Aidha, kiongozi wa chama hicho, Moses Wetangula, anatazamwa na baadhi ya wadau kama mrithi wa Rais William Ruto iwapo atatamatisha hatamu yake. Wanadai Wetangula anahitaji chama imara cha kisiasa kitakachomsaidia kuwarai wananchi na kushirikiana katika kubuni muungano mpya wa kisiasa.