BY VIONA SIMIYU

Wakaazi wa Wadi ya Matulo, eneo la Webuye Magharibi Kaunti ya Bungoma, wameandamana kwa amani wakidai kutengwa katika mgao wa miradi ya maendeleo.Wakiongozwa na Moses Wafula na Andrew Kisaka, wakazi hao walisema maeneo yao yamepuuzwa kwa muda mrefu, hasa katika ukarabati wa barabara.
Wanaeleza kuwa hali mbaya ya barabara imekuwa kikwazo kwa usafiri wa watu na bidhaa, na baadhi ya vijiji vinakuwa vigumu kufikika hasa mvua ikiwa nyingi.Kevin Barasa, mkazi wa Matulo, alisema:“Tumekuwa tukilalamikia hali ya barabara zetu kwa muda mrefu. Tunataka viongozi wasikie kilio chetu na kuhakikisha miradi inafika katika eneo letu bila ubaguzi.”Wakazi hao wamemkosoa pia mwakilishi wao, Stephen Kaiser, wakimtuhumu kutowapa kipaumbele katika ugawaji wa miradi.
Moses Wafula aliongeza:“Tunahitaji uwakilishi unaowajibika. Miradi inapaswa kugawanywa kwa usawa ili kila eneo linufaike na maendeleo.”Wakaazi wamesisitiza kuwa maandamano yao yalikuwa ya amani na lengo lake lilikuwa kuwasilisha mahitaji ya jamii kwa viongozi. Wamewataka viongozi kushirikiana nao kutafuta suluhu ya changamoto za miundombinu badala ya kupuuza malalamiko yao.

Kwa sasa wanasema ukarabati wa barabara ndio kipaumbele kikuu kitakachofungua biashara, usafiri na maendeleo katika Wadi ya Matulo.