
No trespassing background material

BY BRIGID SIKUKU.
Shughuli za usafiri na uchukuzi zilitatizika kwa zaidi ya saa tano katika barabara kuu ya kutoka Misikhu kuelekea Webuye, baada ya wakazi wa soko la Misikhu kuandamana vikali wakilalamikia hali mbaya ya usalama katika eneo hilo. Waandamanaji walifunga barabara kwa mawe na miti, na kuvamia duka moja linalodaiwa kuuza dawa za kulevya kwa vijana.
Hasira za wakazi zilichochewa na kisa cha kusikitisha ambapo mwili wa msichana mdogo wa takriban miaka saba ulipatikana katika mazingira ya kutatanisha sokoni humo. Tukio hilo lilizua ghadhabu kubwa miongoni mwa wananchi, ambao walitaja kuwa ni kilele cha mfululizo wa visa vya kihalifu na ukatili ambavyo vimekuwa vikishuhudiwa kwa muda mrefu.Polisi walipata wakati mgumu kudhibiti maandamano hayo, huku waandamanaji wakitoa madai kuwa maduka kadhaa katika soko hilo yanahusika na biashara haramu ya dawa za kulevya.
Wakazi walisema kuwa vijana wengi wameathirika na matumizi ya mihadarati, hali ambayo imeongeza visa vya uhalifu, uporaji na sasa hata mauaji.Akizungumza na wanahabari katika eneo la tukio, Mwenyekiti wa soko hilo, Cheloti Mukhalusia, pamoja na naibu wake William Mechumo, walisema wamekuwa wakitoa malalamiko kuhusu usalama kwa muda mrefu bila hatua yoyote kuchukuliwa. Walieleza kuwa maandamano hayo ni njia ya mwisho ya kupaza sauti ili serikali iingilie kati.
Wakazi pia walielezea hofu yao kuhusu watu fulani wanaoishi ndani ya soko hilo bila kujulikana shughuli zao halisi, huku wakionekana kuishi maisha ya kifahari yasiyoeleweka. Walitoa wito kwa wamiliki wa nyumba za kupanga kuwa makini na wapangaji wao, na wakaapa kuendesha msako wa kijamii kuwasaka wahalifu.Naibu Kamishena wa eneo la Webuye, Peter Yegon, alithibitisha kisa hicho na kukashifu vikali mauaji ya msichana huyo.
Alisema kuwa uchunguzi wa kina tayari umeanzishwa na kwamba vyombo vya usalama vitahakikisha haki inapatikana. Alitoa hakikisho kuwa kila aliyehusika atakamatwa na kufikishwa mbele ya sheria.Aidha, baadhi ya wananchi waliitaka serikali kuwachunguza maafisa wa usalama walioko eneo hilo, wakidai kuwa kuna uzembe na uhusiano wa karibu baina yao na wahalifu. Neon na Dancun Wanjala, wakazi wa Webuye, walieleza kuwa iwapo maafisa hao hawatabadilishwa, basi hali ya usalama itazidi kudorora.Naibu Kamishena Yegon aliwahakikishia wakazi kuwa serikali haitafumbia macho suala hilo.
Alisema atashirikiana na mashirika ya usalama pamoja na jamii kuhakikisha kuwa hali ya utulivu inarejea. Pia aliahidi kuwa pindi uchunguzi utakapokamilika, hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wale wote watakaopatikana na hatia.