

By Felix Wanjala.
Ni siku ya pili ya ziara ya maendeleo ya Rais William Ruto katika Kaunti ya Narok, ambapo ametumia fursa hiyo kusifu ushirikiano wake wa kisiasa na kiongozi wa ODM, Raila Odinga, akisema hatua hiyo imeimarisha mshikamano wa kitaifa.
Katika ziara hiyo, Naibu wa RaisProfesa Kithure Kindiki aliwakemea vikali baadhi ya viongozi wanaodaiwa kuanza kampeni za mapema, akisema wanapuuza wajibu wao wa kuwahudumia wananchi.
Nao Waziri Mkuu, Musalia Mudavadi, akiwa Othaya, Kaunti ya Nyeri hivi majuzi, aliwahimiza wakazi wa Mlima Kenya kuunga mkono serikali ya Rais Ruto. Alionya kuwa kutoonyesha uungwaji mkono huo kunaweza kuathiri nafasi ya kisiasa ya eneo hilo, ikiwemo wadhifa wa Naibu wa Rais kufikia mwaka wa 2027.
Gavana wa Narok, kwa upande wake, alimrai Rais Ruto kupuuza matamshi ya upinzani, akiahidi kuwa jamii ya eneo hilo itaunga mkono serikali ya Kenya Kwanza ili kufanikisha maendeleo ya wananchi.
Katika sehemu ya Emurrua Dikirr, Rais Ruto alizindua miradi kadhaa ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa barabara nane muhimu kwa gharama ya shilingi bilioni mbili, usambazaji wa umeme kwa nyumba 15,000 na utoaji wa hati miliki kwa wakazi 2,400.