

FELIX WANJALA.
Baadhi ya wakazi kutoka eneo la Magharibi mwa Kenya wamewahimiza viongozi wa kisiasa kuacha malumbano ya kisiasa na badala yake kushirikiana kwa dhati kuwaunga mkono Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi pamoja na Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula.
Wito huu umetolewa kufuatia hali ya sintofahamu miongoni mwa baadhi ya viongozi wa eneo hilo, ambao wameeleza wasiwasi wao kuhusu utekelezaji wa mkataba wa kisiasa uliotiwa saini wakati wa kampeni – mkataba uliodaiwa kuahidi kuwa jamii ya Magharibi ingenufaika kwa asilimia 30 ya mgao wa nafasi serikalini.

Wakazi wanasema badala ya viongozi kuendeleza lawama na migawanyiko, ni vyema wakae meza moja kwa mazungumzo ya pamoja, ili kuweka mikakati ya kuhakikisha ahadi hizo zinatekelezwa, na eneo hilo linapata maendeleo kama maeneo mengine nchini.Haya yanajiri huku Seneta wa Kakamega, Dkt. Boni Khalwale, hivi majuzi akimkosoa Mudavadi kwa madai ya kushindwa kulinda maslahi ya eneo hilo, hasa kufuatia hatua ya serikali kufunga baadhi ya hospitali. Hata hivyo, baadhi ya wakaazi wamesifu hatua hiyo, wakisema ni sehemu ya juhudi za serikali kupambana na ufisadi katika sekta ya afya.