

FELIX WANJALA
Mchakato wa kuwania kiti cha ugavana katika Kaunti ya Bungoma unaendelea kushika kasi huku viongozi wakianza kuweka wazi nia yao ya kuliongoza eneo hilo baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.
Wakazi wa Bungoma wamewataka wanasiasa hao kuendesha kampeni zao kwa heshima, maadili na kuzingatia maslahi ya wananchi, licha ya kuwa bado imesalia miaka miwili kabla ya uchaguzi mkuu ujao.Miongoni mwa waliotangaza azma ya kuwania wadhifa huo ni mwanasiasa Zachariah Barasa, pamoja na aliyekuwa gavana wa pili wa kaunti hiyo, Wycliffe Wangamati, ambaye alihudumu kati ya mwaka 2017 hadi 2022 kupitia chama cha Ford Kenya.Mbunge wa Kimilili, Didmus Barasa, naye ameonyesha nia ya kuwania ugavana.
Barasa amehudumu kama mbunge tangu mwaka 2017, alipoingia kupitia tiketi ya Jubilee,kabla ya kujiunga na chama cha UDA mwaka 2021, ambacho alikitumia kutetea kiti chake mwaka 2022.Mbunge wa Westlands, Timothy Wanyonyi, pia ameweka wazi kuwa ana mpango wa kuwania ugavana Bungoma. Wanyonyi amehudumu kama mbunge tangu mwaka 2013, kupitia chama cha ODM, kinachoongozwa na aliyekuwa waziri mkuu, Raila Odinga.

Wakaazi wamewahimiza wanasiasa wote wanaotamani kuongoza Bungoma kuangazia masuala nyeti yanayowagusa wananchi kama vile elimu, huduma za afya, miundombinu, usalama na ajira.Kwa sasa, kaunti hiyo inaongozwa na Gavana Kenneth Lusaka, anayehudumu muhula wake wa pili baada ya kuchaguliwa tena mwaka 2022 kupitia chama cha Ford Kenya.