
BY FELIX WANJALA
Kiongozi wa chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka, leo ameongoza viongozi wenzake wa upinzani kutembelea nyumbani kwa aliyekuwa Waziri Mkuu wa zamani, Raila Odinga, ili kutoa heshima zao za mwisho na kufariji familia iliyofiwa.
Kundi hilo la viongozi liliwasilisha Ngombe kwa familia ya Odinga kama ishara ya heshima na kutambua mchango mkubwa wa marehemu katika taifa.Kalonzo, ambaye alikuwa amevalia sare za kijani zenye mtindo wa kijeshi, alisema kitendo hicho ni alama ya kumuenzi Raila Odinga, ambaye alimuelezea kama “baba wa maandamano”mtu aliyetoa maisha yake yote kupigania haki na ustawi wa Wakenya wote.
Makamu huyo wa rais wa zamani aliwasili Kang’o ka jaramogi, bila viongozi wengine wakuu wa upinzani, akisisitiza kuwa muungano wao bado uko imara, na kwamba ataendeleza juhudi za hayati Raila Odinga za kupigania haki ya wakenya.Kalonzo amekuwa mshirika wa karibu wa kisiasa wa marehemu Raila Odinga kwa muda mrefu, akiwa amemuunga mkono katika chaguzi kadhaa za urais. Hata hivyo viongozi waliokuwepo walimtaja kama rafiki mkubwa si tu kwa familia bali kwa jamii nzima ya waluo.
Mnamo mwaka 2013, Kalonzo na marehemu Raila,walishirikiana kupitia muungano wa CORD (Coalition for Reforms and Democracy) ambapo Kalonzo alikuwa mgombea mwenza wa Raila.Mwaka 2017, walirejelea ushirikiano wao chini ya NASA (National Super Alliance), Kalonzo akihudumu tena kama mgombea mwenza wa urais.Na mwaka 2022, licha ya kutangaza nia ya kugombea urais, Kalonzo hatimaye alijiunga tena na Raila katika Azimio la Umoja,One Kenya Alliance, ikiwa ni mara ya tatu kumuunga mkono Raila Odinga katika kinyang’anyiro cha urais.