
BY DINA ROSE
Madaktari katika Hospitali ya Rufaa ya Bungoma wameripoti ongezeko la wanawake wajawazito wanaoepuka kujifungulia hospitalini kutokana na kukosa bima ya afya ya SHA, hali inayodaiwa kuchangia vifo vya watoto wachanga pamoja na matatizo ya kiafya kwa watoto.
Daktari Mkuu wa Watoto, Felistus Makokha, alieleza kuwa baadhi ya wajawazito huchagua kwenda kwa wakunga wa jadi (TBA) kwa sababu hawajasajiliwa katika mpango wa bima ya SHA. Alisema hatua hiyo imekuwa na athari kubwa kwa afya ya watoto wachanga.
Kwa mujibu wa Daktari Makokha, kumekuwepo na ongezeko la visa ambapo watoto hufikishwa hospitalini wakiwa katika hali mbaya kutokana na kuchelewa kupata huduma za kitaalamu. Alionya kuwa kuchelewa huko kunaweza kusababisha vifo vya watoto au kuzaliwa kwa watoto wenye ulemavu wa kudumu.
Naye Daktari Maureen Natembeya alibainisha kuwa wanawake wasio na bima ya SHA hujihisi kushawishika kujifungulia nyumbani ili kuepuka gharama za matibabu. Aliongeza kuwa hali hiyo inaweka maisha ya mama na mtoto hatarini.
Daktari Natembeya alikumbusha kuwa mpango wa Linda Mama uliwahi kusaidia kwa kiasi kikubwa kwa kuwawezesha wanawake wengi kujisajili na kupata huduma za afya kwa urahisi, hali iliyosaidia kupunguza changamoto kama hizi hapo awali.
Madaktari hao walitoa wito kwa wanawake wajawazito kuanza kuhudhuria kliniki mapema ili kubaini na kushughulikia matatizo ya ujauzito kwa wakati. Daktari Makokha alisisitiza kuwa hatua hiyo inaweza kusaidia kuzuia watoto kuzaliwa na matatizo ya yanayotokana na kuchelewa kupata huduma.