Serikali ya Kenya imethibitisha kuwa mazungumzo yanaendelea kati yake na Marekani kuhusu mikakati ya kudhibiti mlipuko wa Ebola unaoendelea katika Afrika Mashariki.
BY CYNTHIA ELIZABETH

Serikali ya Kenya imethibitisha kuwa mazungumzo yanaendelea kati yake na Marekani kuhusu mikakati ya kudhibiti mlipuko wa Ebola unaoendelea katika Afrika Mashariki.
Waziri wa Afya, Aden Duale, amesema Kenya inashirikiana na Marekani pamoja na washirika wengine wa kimataifa, lakini hakuthibitisha wala kukataa madai ya kuanzishwa kwa kituo maalum cha uangalizi wa Ebola nchini. Duale alisisitiza kuwa ushirikiano wowote wa afya utazingatia sheria za Kenya na kulinda usalama wa wananchi na wahudumu wa afya.
Ripoti zinaonyesha kuwa mpango wa Marekani unaweza kujumuisha huduma kwa raia wake pekee, hali ambayo imeibua maswali kuhusu masharti ya makubaliano hayo.

Afisa Mkuu Mtendaji wa KEMRI, Elija Songok, amesema serikali imeongeza uwezo wa maabara na upimaji wa magonjwa hatari ili kuimarisha ufuatiliaji na kudhibiti maambukizi. Aidha, KEMRI inaendelea kuboresha miundombinu ya kutenga wagonjwa katika hospitali ya Alupe, iliyotumika wakati wa janga la COVID-19, kama sehemu ya maandalizi ya kukabiliana na milipuko ya magonjwa.
Wakati huo huo, Uganda imeimarisha hatua za udhibiti kwa kufunga baadhi ya mipaka yake na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kutokana na kuenea kwa virusi vya Ebola. Takwimu zinaonyesha kuwa zaidi ya visa 100 vimeripotiwa katika DRC na Uganda, huku juhudi za kikanda zikiendelea kuongezwa.
Mjadala kuhusu ushirikiano wa afya bado unaendelea, huku masuala ya usalama na masharti ya makubaliano yakisalia mezani.