AI-GENERATED IMAGE/TMG

BY FELIX WANJALA
Kauli mbiu ya “Tuko Kadi” imeendelea kushika kasi nchini, ikizua hisia kali hasa miongoni mwa vijana wa kizazi cha Gen Z. Ingawa baadhi ya wanasiasa wameanza kujihusisha na kauli hii, hatua hiyo imewakera vijana waliobuni dhana hiyo kwa lengo la kuhamasisha wenzao kujisajili kama wapiga kura. Vijana wanasisitiza kuwa nguvu ya kizazi chao ndicho kitakacholeta mageuzi makubwa katika uongozi wa taifa.
“Tuko Kadi” ilianza kusambaa kupitia mitandao ya kijamii, na sasa imevuka mipaka ya kidigitali hadi mashinani, ikiwahamasisha vijana kujitokeza kwa wingi kusajili kura. Katika Kaunti ya Bungoma, vijana wametakiwa kuwa mstari wa mbele kupigania mageuzi ya uongozi, wakilalamikia changamoto za ufisadi, ukosefu wa ajira, na uongozi mbovu ambazo zimesababisha eneo hilo kurudi nyuma kimaendeleo.
Wananchi pia wameonyesha mitazamo tofauti huku baadhi wanadai wazazi wanapaswa kuunga mkono juhudi za vijana wao kutaka kushika hatamu za uongozi.Wengine wanahisi kuwa kizazi kipya kina nafasi ya kuondoa viongozi wazembe kupitia kura, badala ya maandamano pekee.
Kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita, vijana wamekuwa wakishiriki maandamano katika maeneo mbalimbali nchini na kuendesha kampeni za mitandaoni wakilenga kushinikiza serikali kutekeleza masuala ya maendeleo. Hata hivyo, sasa wamekumbatia mbinu mpya ya kura wakisema ndiyo silaha pekee ya kuwang’oa viongozi wasio na tija mamlakani.