Baadhi ya watu walikusanyika katika lango la Brandenburg mjini Berlin wakibeba bendera za Israel na mabango yenye picha za mateka zaidi ya 200 wanaoshikiliwa na kundi la wanamgambo wa Hamas tangu kundi hilo lilipofanya uvamizi nchini Israeli Octoba 7.
Rais Frank – walter steinmeier wa Ujerumani aliuambia umati huo kwamba ni jambo lisilovumilika kuona wayahudi wakiishi kwa khofu kwa mara nyingine nchini Ujerumani.
“Kila shambulio dhidi ya wayahudi, taasisi za kiyahudi ni fedheha kwa Ujerumani.” alisema Steinmeier.
Kabla ya hapo, kansela Olaf scholz alishiriki kufungua sinagogi jipya katika mji wa mashariki wa Dessau ambapo alisema ameshangazwa sana na ongezeko la chuki dhidi ya wayahudi tangu kuanza kwa vita kati ya kundi la Hamas na Israel.
Majengo mengi katika mji wa Berlin ambako wanaishi wayahudi yalichorwa milangoni alama ya nyota iliyoko kwenye bendera ya Israel,isitoshe maelfu ya waandamanaji walijitokeza kuwaunga mkono wapalestina na kupinga mauaji yanayofanywa na jeshi laIsrael katika ardhi za wapalestina na kushinikiza Israel iache kuushambulia kwa mabomu ukanda wa Gaza.
Na Samuel Ngoya