Gavana wa Bungoma Kenneth Lusaka amesema katika kipindi cha takribani miaka mitatu ya uongozi wake amefanikisha mageuzi katika sekta za kilimo, elimu, afya na miundomsingi.
BY FELIX WANJALA

Gavana wa Bungoma Kenneth Lusaka amesema katika kipindi cha takribani miaka mitatu ya uongozi wake amefanikisha mageuzi katika sekta za kilimo, elimu, afya na miundomsingi.Akitoa taarifa kuhusu utendakazi wa serikali yake katika bunge la kaunti, Lusaka alijitenga na madai ya ufisadi akisisitiza kuwa mhasibu wa serikali ameweka wazi matumizi ya rasilimali za kaunti, na kwamba lengo lake ni kuboresha maisha ya wakazi.
Lusaka, ambaye awali alikumbana na tuhuma za uvujaji wa fedha mbele ya kamati maalumu ya seneti, alihusishwa na ubadhirifu wa pesa za miradi ikiwemo ujenzi wa uwanja wa Masinde Muliro Kanduyi, makazi ya kifahari ya gavana, na upandaji wa maua mjini Bungoma. Pia alikabiliwa na malalamiko ya dhuluma kwa wafanyakazi wa kaunti.
Hata hivyo, amejivunia kuanzisha mpango wa lishe kwa wanafunzi wa chekechea, kuimarisha sekta ya afya, kujenga nyumba za bei nafuu, masoko na barabara kadhaa.
Kiongozi huyo amekuwa akikabiliwa vikali na Seneta Wafula Wakoli, wakirushiana maneno hadharani kuhusu utendakazi wa kaunti. Lusaka, anayetarajia kutamatisha hatamu zake mwaka ujao, amesema Bungoma inaweza kuendelea kuwa bora iwapo wakazi watachagua kiongozi mwenye maono na ndoto ya kubadilisha maisha ya wananchi.