AI-GENERATED IMAGE/TMG
BY FELIX WANJALA

Vijana wa Bungoma wameandaa matembezi ya amani wakibeba kauli mbiu ya “Tuko Kadi”, wakihamasisha wenzao kujisajili kama wapiga kura kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027. Wanasema lengo lao ni kumaliza uongozi mbaya na kuleta mabadiliko kupitia kura.
Hata hivyo, baadhi ya viongozi wametafsiri kauli hiyo visivyo, jambo ambalo vijana wamelipinga wakisisitiza kuwa nia yao ni kuondoa viongozi wazembe na wafisadi. Wazazi kwa upande wao wametoa wito kwa vijana kujitokeza kwa wingi kuwania nyadhifa za uongozi, wakisema wakati wa kizazi kipya kuongoza umefika.
Wananchi wengine wamelalamikia hali ya Kaunti ya Bungoma, wakidai imerudi nyuma kwa muda mrefu kutokana na ukosefu wa maendeleo, ajira kwa vijana, ufisadi na elimu duni kwa wapiga kura kuhusu umuhimu wa uongozi bora.
Vijana sasa wamekumbatia mbinu mpya ya kujisajili kama wapiga kura chini ya mpango wa “Tuko Kadi”, wakiahidi kutumia kura kuwapigia viongozi wenye nia ya kuleta maendeleo. Kauli hii, iliyoanza kusambaa mitandaoni wiki mbili zilizopita, inalenga kuhakikisha viongozi wenye historia ya ufisadi, dhuluma na kukiuka haki za binadamu hawapati nafasi ya kuongoza tena.