BY FELIX WANJALA

ODM Yazidi Kugawanyika: Sifuna na Oburu Wavutana Kuhusu Mustakabali wa 2027
Mazungumzo ya maridhiano ndani ya chama cha ODM yanaonekana kuyumba, huku pande mbili hasimu zikionyesha nia tofauti kuelekea siasa za mwaka wa 2027.
Katibu Mkuu wa ODM na Seneta wa Nairobi, Edwin Sifuna, ameibuka kuwa mpinzani mkuu wa kiongozi wa sasa wa chama, Oburu Oginga. Sifuna ameendelea kupinga sera za serikali, ilhali Oburu akionekana kuzisifia kwa lengo la kubuni muungano mpya wa kisiasa.
Tofauti zao ziliibuka wazi katika mikutano ya kitaifa ya wanachama wa NDC jijini Nairobi, ambapo kila mmoja aliendesha mkutano wake na kundi lake. Mkutano wa Oburu ulisisitiza nidhamu na utiifu kwa chama, akionya kuwa yeyote atakayekwenda kinyume na maamuzi ya chama atatimuliwa. Kauli hiyo ilizua mjadala, baadhi wakikumbusha kuwa chini ya Hayati Raila Odinga, ODM ilikuwa ikisikiliza maoni ya wanachama hata kama yalipingana na msimamo wa chama.
Kwa upande wake, Sifuna amesisitiza kuwa hawezi kushirikiana na serikali na lengo lake ni kutetea haki za Wakenya. Amedai kuwa katika siasa za 2027 yuko tayari kushirikiana na upinzani kumng’oa rais mamlakani. Ameonekana akiendesha mikutano katika maeneo mbalimbali ikiwemo Busia, Kitengela, Kakamega, Narok na sasa Mombasa, akisisitiza kauli ile ile.
Maeneo haya ambayo kwa muda mrefu yamekuwa ngome ya ODM, sasa yamekuwa uwanja wa Sifuna kutathmini iwapo wafuasi watabaki upande wake ama kujiunga na mrengo wa Linda Ground.
Matukio haya yanaendelea kuchochea nyufa zaidi ndani ya ODM, huku wachambuzi wakionya kuwa huenda yakavuruga mazungumzo ya maridhiano kati ya mrengo wa Linda Ground na chama cha UDA, na hatimaye kuathiri siasa za mwaka wa 2027.